Wiki hii ni maadhimisho ya mwaka ilisitisha wanawake kuhudhuria masomo katika taasisi za elimu ya juu za umma na binafsi, na kuifanya nchi maskini ya Afghanistan kuwa ni nchi pekee duniani kupiga marufuku kwa wasichana kupata elimu ya kuanzia darasa la saba na kuendelea.
Thomas West, mwakilishi maalum wa Marekani kwa Afghanistan, ameiita marufuku hiyo ya mwaka mzima katika elimu ya chuo kikuu “haina utetezi.”
Aliandika katika mtandao wa X, uliokuwa unajulikana kama Twitter, kuwa mgogoro unaolikumba taifa la Asia Kusini “linahitaji kizazi siku za usoni cha wanawake madaktari, wahandisi, viongozi wa biashara, na waalimu ili kukua na kufanikiwa na kujitegemea."
“Kwa maslahi ya mustakbali wa Afghanistan na maslahi yetu katika kanda iliyo imara, ni lazima kuwepo fursa ya elimu kwa wanawake katika ngazi zote katika misingi ya vipaumbele vyetu,” West aliongeza kusema.
Wataliban walirejea madarakani mwezi Agosti 2021 na kuweka tafsiri yao kali ya sheria ya Kiislam, na kuweka masharti jumla kwa wanawake wa Afghanistan kuingia vyuoni kupata elimu na kufanya kazi.
Watawala wa Kiislam wamepuuza ukosoaji wa kimataifa juu ya sera zao, wakisema wanakwenda sambamba na utamaduni wao na Sheria za Kiislam.
Rina Amiri, mwakilishi maalum wa Marekani kwa wanawake, wasichana wa Afghansitan na haki za binadamu, alihoji madai ya Taliban Alhamisi na kuwakosoa viongozi walioko madarakani kwa kuwaondolea nusu ya wananchi wa nchi hiyo haki zao za msingi.
“Sote lazima tusimame pamoja na watu wa Afghanistan, hususan wanawake na wasichana, wakati wakitueleza tupinge sera hizi na kukumbuka kuwa hizi siyo sera zinazotokana na utamaduni wa Afghanistan, bali ni itikadi za Taliban,” Amiri aliandika katika akaunti ya X.
Waziri wa Elimu ya Juu wa utawala wa Taliban Nada Mohammad Nadim alisema katika sherehe za mahafali kwa mamia ya wanafunzi wa kiume katika chuo kikuu kikubwa katika mji mkuu, Kabul, kuwa serikali yake ina nia ya dhati ya kuendeleza elimu nchini.
Nadim hakufafanua au kujadili masuala yanayo husiana na elimu ya juu kwa wanawake, ambayo yalisitishwa na wizara yake mwaka 2022.
“Wageni wanatoa mapendekezo kwa maendeleo ya Afghanistan; ukweli, hawataki maendeleo ya nchi hii,” waziri huyo alisema akijibu ukosoaji wa kimataifa.
Shirika la hisani la Canadian Women for Women in Afghanistsan, ililaumu kile ilichokiita “sera za ubaguzi wa kijinsia” za Taliban zinazo changia moja kwa moja kwa kuzorota hali za kibinadamu nchini humo, zikirudi nyuma miaka kadhaa ya vita na majanga ya kiasili.
Umoja wa Mataifa unasema takriban theluthi mbili ya raia wa Afghanistan wanahitaji chakula na misaada mingine.
Ripoti ya mwandishi wa VOA Ayaz Gul.
Forum