Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Septemba 28, 2023 Local time: 08:06

WHO : Tahadhari mpya yahamasisha misaada kudhibiti Ebola DRC


Muuguzi akimpa mtu chanjo dhidi ya Ebola nje ya kituo cha afya cha Afia Himbi Julai 15, 2019, Goma.

Shirika la Afya Duniani, WHO, limetangaza Jumatano, kuwa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kwenye majimbo ya Kivu kaskazini na Ituri kuwa janga la dharura ya kiafya inayohitaji kuangaziwa kimataifa.

Tangazo la Ebola kuwa dharura ya kimataifa sasa linafungua mlango wa misaada na juhudi zinazohitajika kukabiliana nao. Hata hivyo mwenyeiti wa kamati ya dharura Robert Steffen anatahadharisha dhidi ya kutoelewa maana halisi ya hatua hiyo.

Hii ni dharura ya kieneo na wala siyo tishio la ulimwengu. Hata hivyo tumebadili mtazamo kutokana na Ebola kupatikana mji wa Goma ambao ni kiingilio cha kimataifa licha ya kuwa hakuna visa vipya viivyoripotiwa, amesema

Jumapili iliopita kesi ya kwanza ya Ebola ilitangazwa Goma, mji wenye wakazi takriban milioni 2 na tangu wakati huo mchungaji alieambukizwa tayari amekufa.

Steffen amesema kuwa kuzuka kwa maambukizi mapya mjini Beni ambapo huko nyuma ilikuwa kitovu cha ugonjwa huo, pamoja na kuuwawa kwa wahudumu wawili wa Ebola ni baadhi ya mambo yaliopelekea uamuzi wa kamati yake.

Mratibu mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus anasema kuwa bado kuna hatari kubwa ya kuenea kwa maambukizi nchini humo kinyume na kuenea kwenye mataifa ya kieneo.

Ameongeza kusema kuwa licha ya kamati kutagaza janga hilo kuwa la kimataifa, WHO halijatoa makataa yoyote ya kusafiri au kufanya biashara.

Hatua hio huenda ikahujumu vita dhidi ya Ebola. Kufunga mipaka kutaathiri maisha ya watu wengi wanaovuka kila siku kutokana na sababu mbali mbali kama vile biashara, kutembela jamii na kutafuta elimu.

Tangu mlipuko wa Ebola ulipotangazwa Agosti mosi mwaka 2018, WHO linasema kumekuwa na zaidi ya visa 2,500 pamoja na vifo 1,670.

Huu ndiyo mlipiko wa nne katika kipindi cha miongo minne nchini DRC. Mlipuko wa sasa umeorodheshwa kuwa wa pili kwa ukubwa baada ya ule wa Afrika Magharibi wa 2014, uliouwa zaidi ya watu 11,300.

WHO limeonya kuwa ukosefu wa usalama kwenye majimbo ya Kivu kaskazini na Ituri pamoja na misaada midogo ya kifedha ya kimataifa kuwa maswala yanayohujumu juhudi za kuangamiza ugonjwa huo.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG