Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Mei 02, 2024 Local time: 16:02

WHO yatahadharisha juu ya uwezekano wa Ebola kushindwa kudhibitiwa DRC


Kituo cha kushughulikia waliopatwa na virusi vya Ebola Beni, DRC.
Kituo cha kushughulikia waliopatwa na virusi vya Ebola Beni, DRC.

Mashambulizi ya kutumia silaha, kuenea kwa habari potofu na ukosefu wa fedha vimeendelea kuchangia katika vizingiti vilivyoko katika kukabiliana na mlipuko wa maradhi ya Ebola upande wa kaskazini mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) likitahadharisha kunauwezekano ugonjwa huo ukashindwa kudhibitiwa.

Kukosekana usalama kumefanya timu za wanaokabiliana na maradhi hayo “kushindwa kutekeleza tahadhari muhimu na pia kushindwa kufikisha matibabu na chanjo muhimu,” WHO imeripoti siku ya Ijumaa katika taarifa yake ya hivi karibuni juu ya mlipuko uliyokuwa umethibitishwa Agosti 2018.

WHO imetahadharisha iwapo “hakutakuwa na azma ya makusudi kwa vikundi vyote kusitisha mashambulizi, itakuwa vigumu kwa mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa Ebola kuendelea kudhibitwa katika eneo la Kaskazini mwa Kivu na majimbo ya Ituri.

Ugonjwa huo unaweza kuenea katika maeneo mengine ya nchi hiyo na kuvuka mipaka katika nchi za jirani ikiwemo Uganda, Rwanda na Sudan Kusini, WHO imeeleza uwezekano huo.

Mwezi huu peke yake kumekuwa na vikwazo kutokana na mashambulizi ya uvunjifu wa amani kwa timu ya wanaoshughulika na mazishi ya waliokufa kwa Ebola katika mji wa Katwa na mapambano ya bunduki kati ya wanamgambo wasiopungua 50 wenye silaha na vikosi vya usalama katika mji wa Butembo, imesema WHO.

Waombolezaji pia walimzika Richard Valery Mouzoko Kiboung, miaka 41, Daktari kutoka Cameroon aliyekuwa akifanya kazi na WHO ambaye aliuawa Aprili 19 na pia ikiwa ni sehemu ya shughuli zake alikuwa akikutana na wafanyakazi walioko mstari wa mbele kupambana na ugonjwa huu katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Butembo.

Alhamisi, mwandishi wa VOA Butembo aliweza kuziona nakala za barua, zilizokuwa zimekandamizwa na mawe njiani na nyingine kubandikwa kwenye majengo huko na katika jamii nyingine huko Kivu Kaskazini.

Barua hizo zikiwa zimeandikwa kwa Kiswahili na zikitoka kwa wapiganaji wa Mai-Mai, zimewaonya polisi, wanajeshi na umma kwa ujumla kuacha kuwasaidia wanaokabiliana na ugonjwa wa Ebola au vituo vya matibabu.

Anderson Djumah, ambaye mtoto wake mwenye umri wa miaka 10 anatibiwa kutokana na maradhi ya Ebola huko katika hospitali ya Butemba, amelalamika kuwa “kukosekana usalama kumeongeza mateso zaidi.”

Sasa hata vituo vya kutibu Ebola vinalengwa na washambuliaji hao. Tuna wasiwasi. Ebola inauwa watu wengi. Bado tunamatumaini kuwa serikali itaweza kutulinda,” amesema.

“… lakini baadhi ya watu ambao wanaugua maradhi ya Ebola wanakimbilia maeneo mengine kuokoa maisha yao na hivi sasa wanaeneza maambukizi.”

Uvunjifu wa amani unafanya watu wakimbilia kutafuta hifadhi na hivyo shughuli za matibabu zinavurugwa kama vile kufuatilia wale walioambukizwa, kutoa chanjo na maeneo salama dhidi ya maambukizi ya maziko, na hilo linatoa muda na nafasi kwa virusi kuenea katika jamii na kufanya wahanga kuongezeka,” Jessica Ilunga, msemaji mwanamama wa wizara ya afya DRC ameiambia VOA.

“Kila wakati tunapokuwa na matukio ya uvunjifu wa amani, idadi ya wagonjwa na vifo inaongezeka,” Ilunga amesema.

Wizara ya afya inayoongoza mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola kwa msaada wa WHO imeripoti kuwa jumla ya wagonjwa 1,600 mpaka kufikia Jumatano, kati yao 1,534 wamethibitishwa kuwa na virusi vya Ebola na wengine 66 wanadhaniwa wanavyo.

Mlipuko mbaya zaidi wa pili kuliko yote wa Ebola tayari umeuwa watu 1,069. Ule wa mwaka 2014-15 Africa Magharibi uliuwa zaidi ya watu 11,000.

XS
SM
MD
LG