Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Mei 31, 2024 Local time: 00:28

UN yatangaza mikakati mipya kukabiliana na Ebola DRC


Maafisa wa afya wakikabiliana na ugonjwa wa Ebola nchini DRC.
Maafisa wa afya wakikabiliana na ugonjwa wa Ebola nchini DRC.

Umoja wa Mataifa umetangaza kubuniwa kwa mikakati mipya ya kukabiliana na kuenea kwa ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)..

Ripoti ya mpango huo mpya imewasilishwa wakati wa mkutano mkuu wa afya duniani unaofanyika mjini Geneva, Uswizi.

Mpango huo utahusisha maafisa wa ngazi za juu ambao wataratibu operesheni za Umoja wa mataifa na wahusika wengine wa kimataifa katika kukabiliana na kuenea kwa virusi hivyo hatari.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amewateua maafisa wawili waandamizi, ambao amesema wana tajriba kubwa za kuwawezesha kuongoza operesheni hizo.

David Gressly atasimamia uratibu wa masuala ya dharura huku akishirikana kwa karibu na naibu mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani anayehusika na masuala ya dharura za kiafya, Ibrahima Sose Fall.

Fall amekuwa akiongoza operesheni za kukabiliana na ugonjwa huo katika mji wa Butembo, Mashariki mwa DRC, tangu mwezi Machi mwaka huu.

FILE - David Gressly, afisa wa ngazi ya juu ambaye ataongoza mikakati mipya ya kukabiliana na kuenea kwa Ebola nchini DRC.
FILE - David Gressly, afisa wa ngazi ya juu ambaye ataongoza mikakati mipya ya kukabiliana na kuenea kwa Ebola nchini DRC.

Kwa mujibu wa msemaji WHO, Tarik Jasa-veric, Umoja wa mataiafa sasa utashirikiana kwa karibu Zaidi na serikali ya DRC na wadau wengine, ili kuondoa hatari ya ugonjwa huo kufika viwango visivyodhibitika.

Haya yanajiri huku ugonjwa huo ukiwa umesababisha vifo vya takriban watu 1,200, tangu mlipuko wake kuripotiwa miezi kumi iliyopita katika majimbo yanayokumbwa na machafuko, ya Kivu Kaskazini na Ituri, yaliyo Mashariki mwa nchi hiyo.

Katika siku za karibumni, wasiwasi umeongezeka kwamba virusi hivyo huenda vikasambaa katika maeneo mengine ya nchi na hata kwenye nchi jirani.

XS
SM
MD
LG