Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Julai 15, 2024 Local time: 05:51

Marekani, Russia zakinzana kuhusu ghasia zenye msimamo mkali kanda ya sahel


US Russia Arms Control
US Russia Arms Control

Marekani imewashutumu wakandarasi wa kijeshi wanaoungwa mkono na Russia kwa kuingilia kati masuala ya ndani ya nchi za Kiafrika na “kuongeza uwezekano wa kuzidisha matukio ya ghasia zenye msimamo mkali” katika kanda ya Sahel.

Kutokana na wakandarasi hoa wa Russia, Kanda ya Sahel inakabiliwa na ongezeko la mashambulizi, tuhuma ambazo Russia imekanusha.

Naibu Balozi wa Marekani Richard Mills Jumanne alilikosoa kundi la Wagner katika mkutano wa Baraza la Usalama la UN kuhusu Afrika Magharibi na Sahel.

Aliwatuhumu askari wa miamvuli kwa kushindwa kushughulikia tishio la makundi yenye silaha, yakiiba rasilmali ya nchi hizo, wakifanya vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu na kuhatarisha usalama na amani ya walinzi wa amani wa UN na wafanyakazi wake.

Richard Mills
Richard Mills

Mwanadiplomasia wa kisiasa wa Ufaransa, Isis Jaraud-Darnault, alimuunga mkono Mills, akisema kwamba “utaratibu” uliotumia na mamluki wa kikundi cha Wagner umethibitisha “hakiwezi kabisa kupambana na ugaidi”.

Mwanadiplomasia huyo ameeleza kuwa “vitendo vya uhalifu” na athari za uharibifu wa shughuli zao na ukiukaji wa haki za binadamu, ikiwemo madai ya mauaji ya zaidi ya raia 30 huko Mali, na wizi wa rasilimali za asili.

Naibu Balozi wa Uingereza James Kariuki alieleza kuharibika kwa hali ya usalama nchini Mali, Burkina Faso, Nigeria na Bonde la Ziwa Chad, na hofu ya kukosekana utulivu inayoenea katika nchi za pwani ya Afrika Magharibi.

“Huwezi kupuuzia namna kikundi cha Wagner kinavyo hujumu katika kanda hiyo. Wao ni sehemu ya tatizo, na siyo suluhisho,” aliliambia baraza hilo.

James Kariuki
James Kariuki

Naibu Balozi wa Russia Anna Evstigneeva alitupilia mbali kile alichokiita ni majaribio ya “kuchafua msaada wa Russia kwa Mali”, ambako Moscow ina mkataba wa pande mbili wa kuisaidia serikali ya mpito, “na katika nchi nyingine za Afrika”.

“Baadhi ya nchi leo kwa mara nyingine tena zimetangaza kuwa Russia inaelekea kuiba na kupora rasilmali za Afrika na inasaidia kukua kwa tishio la ugaidi,” alisema, akizishutumu nchi ambazo hazikutajwa kwa kufanya kitu hicho hicho “kote ulimwenguni na Afrika”. Hususan katika nchi jirani ya Libya, ambayo imeliyumbisha eneo lote.

“Tuhuma dhidi ya Russia zinashangaza, kwa fikra ya kawaida,” na zinawahujumu viongozi wa kiafrika ambao wanajaribu kutatua matatizo yao na kuamua nani wanataka kushirikiana naye, alisema mwanamama huyo.

Evstigneeva hakutaja jina la kikundi cha Wagner. Kikundi hicho kinaendeshwa na Yevgeny Prigozhin, mshirika wa karibu wa Rais wa Russia Vladimir Putin, na mamluki wake wanatuhumiwa na nchi za Magharibi na wataalamu wa UN kuhusika na namna mbalimbali za unyanyasaji wa haki za binadamu kote Afrika, ikiwemo Jamhuri ya Afrika ya Kati, Libya na Mali.

Chanzo cha habari hii ni kituo cha habari cha Al Jazeera.

XS
SM
MD
LG