Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 21, 2025 Local time: 21:30

Afghanistan: Mamlaka zenye msimamo mkali zawanyonga hadharani watu wawili


Mullah Hibatullah Akhundzada
Mullah Hibatullah Akhundzada

Mamlaka zenye msimamo mkali Afghanistan  Alhamisi zimewanyonga hadharani  watu wawili ambao wamekutwa na hatia ya mauaji katika matukio mawili tofauti.

Mahakama ya Juu ya Taliban ilisema watanyongwa, kwa kupigwa risasi ambapo ilitekelezwa katika uwanja wa mpira katika mji wa kusini mashariki wa Ghazni.

Idadi kubwa ya maafisa wa mahakama na serikali, na pia wakazi wa eneo hilo, walishuhudia tukio hilo, lakini hakuna mtu aliyeruhusiwa kuleta simu za mkononi au kamera uwanjani.

Taarifa hiyo ya mahakama ilisema wawili hao waliohukumiwa kifo kesi zao zilisikilizwa na walikutwa na hatia kwa makosa ya kuwachoma kisu na kuwaua watu wawili. Iliongeza kuwa amri ya mahakama ilitekelezwa baada ya kiongozi wa juu wa Taliban, Hibatullah Akhundzada, kuidhinisha.

Wataliban wameua watu wanne na kuwapiga viboko wengine 350, wakiwemo wanawake, mbele ya mamia ya watazamaji tangu walipochukua tena madaraka mwezi Agosti 2021, na kuanzisha utekelezaji wa tafsiri ya sheria kali za Kiislam.

Waathirika wanawake wengi wao walituhumiwa kwa uhalifu kama vile uzinifu na kukimbia majumbani mwao.

Wanawake wa Afghanistan wakisubiri kupokea msaada wa chakula.
Wanawake wa Afghanistan wakisubiri kupokea msaada wa chakula.

Umoja wa Mataifa umekosoa adhabu hizo na kusema zinakiuka haki za binadamu, wakisema zinakwenda kinyume na sheria za kimataifa na lazima zisitishwe.

Wataliban wametupilia mbali ukosoaji huo, wakisema mfumo wao wa sheria za uhalifu na uongozi wao kwa jumla umejikita katika kanuni za Kiislam na miongozo yake.

Kupigwa viboko na kunyongwa ilikuwa ni desturi ya kawaida chini ya utawala wa Taliban uliopita nchini Afghanistan tangu mwaka 1996 hadi 2001.

Mamlaka nchini Afghanistan zimeweka masharti ya jumla dhidi ya haki za wanawake kupata elimu na maisha yao katika jamii. Wamewazuia wageni wanawake kufika katika viwanja vya wazi na nyumba za mazoezi na kuwakataza watoto wa kike kuendelea na masomo baada ya kumaliza darasa la sita.

Wataliban wamepuuza malalamiko ya kimataifa na wito wa kuondoa vizuizi dhidi kwa wanawake.

Vitendo vyao kwa wanawake ndiyo sababu kuu iliyoyazuia mataifa ya kigeni kuutambua utawala wa Taliban huko Kabul.

Jopo la wataalam wa UN wiki hii wamezitaka nchi nyingine kutambua rasmi “ubaguzi wa kijinsia” kama uhalifu dhidi ya ubinadamu, ikigusia ukandamizaji wa wanawake na wasichana unaofanywa chini ya utawala kama huu wa Taliban nchini Afghanistan.

Ripoti ya mwandishi wa VOA Ayaz Gul.


Forum

XS
SM
MD
LG