Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Septemba 10, 2024 Local time: 09:59

Umasikini Uganda : Museveni awalaumu mafisadi, upinzani


Rais Yoweri Museveni
Rais Yoweri Museveni

Rais wa Uganda amesema kuwa hakuna nchi nyingine duniani iliyoweza kuwa na uchumi unaokua haraka kama Uganda, ukitoa Ujerumani, lakini juhudi za kuleta maendeleo Uganda zinakwamishwa na idadi kubwa ya mafisadi serikalini na wanasiasa wa upinzani.

Amedai kuwa kama Uchumi wa Uganda ungeendelea kukua kwa kasi hiyo, hivi leo ingekuwa tajiri hata kuliko Marekani.

Yoweri Museveni hata hivyo anasema ndoto yake ya kuitajirisha Uganda bado iko hai, akiongeza kuwa hivi sasa, kuna wimbi la wawekezaji wanaoingia nchini humo kwa wingi.

Katika hotuba yake kwa taifa, kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha 2018/2019, ameeleza kuwa kwa sasa, Uganda ingekuwa miongoni mwa nchi mbili tajiri zaidi duniani, lakini ufisadi, uongozi mbaya uliomtangulia, siasa za upinzani na kukosa kutekeleza miradi muhimu kwa wakati, vimefanya nchi hiyo kusalia katika orodha ya nchi masikini.

Museveni amesema tatizo kubwa la Uganda ni mafisadi, wanaoiba mali ya taifa.

“Hakuna nchi yoyote ya Ulaya hata Marekani ambayo uchumi wake ulikua kwa kasi kama Uganda kwa muda wa miongo mitatu, isipokuwa Ujerumani ambayo kati ya mwaka 1950 na 1980kwa asilimia 3.8,” amesema Museveni

Japo raia wengi wa Uganda na wakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa jumla, walitarajia kwamba Museveni angezungumzia suala la mgogoro kati ya Uganda na Rwanda, amekwepa kulitaja, na badala yake kusisitiza kwamba wanajeshi wa usalama wapo imara kila saa kulinda Uganda na mipaka yake yote, iwe nchi kavu, angani au majini.

Sekta za viwanda, mafuta na gesi, utalii, nshati, ujenzi wa barabara, reli ya kisasa SGR, na kilimo ndio masuala muhimu Museveni anaamini nchi yake inastahili kuangazia, akiahidi utafiti wa kipekee unaofanywa na wanasayansi wake, wa kuhakikisha kwamba kupe wanakufa wenyewe wanapofyonza damu ya ng’ombe na mifugo wengine.

Hata hivyo, hakukosa kuwashambulia wapinzani wake, hasa chama cha DP, ambacho kimeonekana kuwavutia wanamziki maarufu Bobi Wine na Jose Chameleon ambaye amekiacha chama cha Museveni cha NRM, na kwamba hakuna chama cha upinzani Uganda kinaweza kujisimamisha bila Museveni.

“Usiniambie kwamba huwezi kutumikia watu wako kama haupo serikalini. Hiyo ni takataka na hauna maana yoyote. Nakwambia nikiwa na mamlaka hayo kwa sababu nilikuwa upinzani. Wengine wanatembea huku na huku wakiinua miguu juu kwamba wako DP. Hakuna DP bila Museveni. Nilikuwa huko na ninawajua wote,” ameeleza Museveni

Hotuba ya leo, inatoa fursa ya ufunguzi wa kikao cha nne cha bunge la Uganda, mwisho wa mwaka wa fedha 2018/2019, na kuanza kwa mwaka wa fedha 2019/2010, baada ya bajeti kusomwa Alhamisi wiki ijayo.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, Washington, DC

XS
SM
MD
LG