Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Septemba 15, 2024 Local time: 13:55

Bobi Wine na Besigye waungana kupambana na Museveni 2021


Sebestian Coe rais wa IAAF na Rais Yoweri Museveni kwenye ufunguzi wa Cross Country 2017
Sebestian Coe rais wa IAAF na Rais Yoweri Museveni kwenye ufunguzi wa Cross Country 2017

Kiongozi wa upinzani Kizza Besigye na Mbunge Robert Kyagulani maarufu Bobi Wine nchini Uganda, wamekubaliana kufanya kazi kwa pamoja ili kukishinda chama kilichoko madarakani cha NRM cha Rais Yoweri Museveni kwenye uchaguzi 2021.

Taarifa hiyo imetolewa Jumatano kwa vyombo vya habari na wasemaji wa vuguvugu la wanaharakati wa makundi ya People’s Power la Bobi Wine na la People's government la Besigye.

Wakizungumza na vyombo vya habari Jumatano mjini Kampala, msemaji wa People’s Power Joel Ssenyonyi na msemaji wa vuguvugu la mapinduzi People’s government la Kizza Besigye, Mbunge Betty Nambooze wamesema pande mbili za vuguvugu hilo zitafanya harakati za pamoja ili kumzuia Rais Museveni aliye madarakani tangu mwaka 1986 asishinde uchaguzi wa 2021.

“Makundi mawili haya yana shughuli tofauti na tutaendelea kuzifanyia kazi na mara kwa mara tutafanya shughuli za pamoja”, amesema Ssenyonyi, msemaji wa People’s power inayoongozwa na Bobi Wine.

Jumanne, Bobi Wine alikiri kwamba vuguvugu lake limekuwa likifanya mikutano na vyama tofauti vya siasa wakiwemo wapinzani wa ndani ya chama tawala cha NRM cha Yoweri Museveni na chama cha Kizza Besigye.

Mbunge Betty Nambooze amesema katika mikutano kati ya wapinzani wa Rais Museveni, suala la kuwa na mgombea moja kwenye uchaguzi ujao lilijadiliwa, na lengo hasa ni kurejesha utawala unaoheshimu uhuru wa wanainchi wote wa Uganda.

Nambooze ameongeza kuwa, lengo kuu ni kumuondoa rais Museveni hata kabla ya uchaguzi wa 2021, na iwapo mpambano huo utahitaji kuwa na mgombea mmoja atakaewakilisha upinzani ili ufikie lengo hilo basi wapinzani hawatokua na budi kumteua mgombea mmoja.

Mchambuzi wa siasa za Uganda Akol Amazima ameiambia Sauti ya Amerika kwamba kuungana kwa Besigye na Bobi Wine bila shaka, kutampa changamoto kubwa rais Museveni.

Pamoja na hivo, Amazima anasema ili upinzani uweze kumshinda rais Museveni, kuna ulazima wamteuwe mgombea mwenye uzoefu wa kisiasa.

Baada ya kipengele cha katiba kilichomzuia mtu mwenye umri wa miaka 75 kugombea urais kuondolewa na bunge la Uganda, Rais Museveni aliye na umri wa miaka 74 sasa anaruhusiwa kugombea tena kwenye uchaguzi ujao baada ya kutumikia kwa muda wa miaka 33. Tayari chama chake cha NRM kimekwisha kumtangaza kama mgombea pekee atakaye wakilisha chama hicho kwenye uchaguzi wa 2021.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Patrick Nduwimana, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG