Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 26, 2022 Local time: 14:55

Uganda yaionya EU


Mwanaharakati anayepinga kuongezwa umri wa kuruhusiwa kugombea nafasi ya urais nchini Uganda akikamatwa na askari kanzu.

Serikali ya Uganda imelionya bunge la Umoja wa Ulaya ( EU), Jumatatu ikilitaka kukoma kuingilia masuala ya uongozi wake pamoja na kuacha kutoa masharti kwa viongozi wa Uganda juu ya haki za binadamu.

Utawala wa Uganda unadai kwamba bunge la EU limekasirishwa na msimamo mkali wa Uganda dhidi ya ushoga, na kuongeza kwamba haitatatizwa na vitisho vya kutopewa msaada wa kifedha wala silaha.

Bunge la EU, Alhamisi iliyopita, ilijadili juu ya dhuluma za kibinadamu zinazodaiwa kutekelezwa na utawala wa Uganda.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari baadhi ya maamuzi kati ya 14 yaliyo tolewa na Bunge hilo yameitaka serikali ya Uganda, kuheshimu uhuru wa bunge, kuheshimu haki za kibinadamu, na kufuta mashtaka ya uhaini dhidi ya mbunge Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, na wabunge wenzake, likisema kwamba mashtaka hayo ni ya kupandikiza.

Tamko la Bunge la EU

Tamko la Bunge la EU limesema : "Hatuwezi kukosa kuzingatia kile kinachoendela Uganda. Hakuna uhuru. Kuna dikteta aliye madarakani na amekuwepo wa muda mrefu.

Limeendelea kueleza kuwa : "Hataki upinzani wala mtu yeyote anaye mkosoa. Yeyote anaye mkosoa anazuiliwa gerezani. Hata waandishi wa habari nao wanadhulumiwa. Tunastahili kuangazia uhusiano wetu wa maendeleo na pesa tunazotoa kwa Uganda, hadi haki za kibinadamu na mfumo wa demokraisa vitakapo heshimiwa.

Serikali ya Uganda yajibu

Msemaji wa serikali ya Uganda Ofwono Opondo, amesema kwamba Uganda haiogopi kuharibu uhusiano wake na umoja wa ulaya na kwamba ipo tayari kwa vita ilivyovitaka kama vita vya haki.

Opondo anadai kwamba EU ina hasira na Uganda kwa sababu nchi hiyo ya Afrika Mashariki ina msimamo mkali dhidi ya ushoga, na kwamba maamuzi ya bunge la ulaya hayatakubalika nchini Uganda.

Ameongeza kuwa EU ina tamaa ya kupata rasilmali za bara la Afrika, Uganda ikiwa mojawapo, na kwa sababu Uganda imeonyesha ushirikiano wake na nchi nyingine, ndio maana bunge hilo limechukua msimamo wa kuikosoa.

Kama nchi, hatuhitaji kufundishwa na EU. Wao wako nchni Congo, hatuoni mabadiliko huko. Wako Togo, Gabon, Libya, Iraq, Syria, lakini hatuoni mabadiliko. Lengo lao ni kuharibu Afrika na kupora mali zetu.

EU yasema haitaivumilia Uganda

Bunge la umoja wa ulaya lilikubaliana kwamba halitaendelea kutumia hoja ya Uganda kuwapa hifadhi wakimbizi kutoka nchini jirani, kunyamaza, huku raia wa Uganda wenyewe, hasa wapinzani wa rais Museveni, wakiendelea kuuawa, kupigwa na kuumizwa, huku wakiwa hawana uhuru wa kujieleza.

Bunge hilo vile vile lina wasiwasi kwamba dhuluma dhidi ya raia wa Uganda zitaendelea katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, wakati Museveni anapo jitayarisha kusalia madarakani baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2021.

Wakati mzozo kati ya Uganda na umoja wa ulaya ukionekana kufukuta, serikali ya Uganda imeonya waandishi wa habari inayodai wanalipwa na nchi za nje ili kueneza picha ya machafuko na dhuluma vinavyo daiwa kutekelezwa na Uganda.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, VOA, Washingtn, DC.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG