Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 05, 2022 Local time: 01:04

Bobi Wine anyimwa dhamana, azuiliwa gerezani - Mawakili


Wafuasi wa Bobi Wine wakitawanywa na polisi katika eneo la Busabala, ambako alikuwa anatarajiwa kuongea na waandishi wa habari, Aprili 22, 2019.

Mbunge na mwanamuziki maarufu nchini Uganda Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, anazuiliwa katika Gereza la Luzira, Jijini Kampala, baada ya kukamatwa na polisi Jumatatu, asubuhi.

Polisi walimkamata Bobi Wine, akiwa safarini kuelekea makao makuu ya upelelezi jijini Kampala, alikotakiwa kuhojiwa kuhusiana na madai ya polisi ya kwamba alikuwa anachochea ghasia wakati wa maadimisho ya Pasaka.

Wafuasi wajitokeza

Wakati huohuo wafuasi wa Bobi Wine walikuwa wanaimba nyimbo za kuhamasisha kupinga kukamatwa kwa mwanamuziki huyo na kuonyesha nguvu ya raia, nje ya mahakama iliyoko Barabara ya Buganda Jijini Kampala, baada ya Jaji Esther Nahirya, kuamuru kwamba Bobi Wine azuilie katika gereza kuu la Luzira.

Hayo yote yalijiri baada ya kusomewa mashataka ya kufanya maandamano kupinga kodi ya serikali kwa mitandao ya kijamii maarufu Uganda kama OTT, makosa anayodaiwa kufanya akiwa na wenzake ambao hawakuwa mahakamani, Julai 11 mwaka uliopita 2018.

Bobi Wine aonekana mwenye tabasamu

Akionekana mwenye tabasamu, ndani ya basi la magereza, lenye vizuizi vya chuma, Bobi wine aliwapungia wafuasi wake mkono, waliokuwa wakiimba wimbo aliotunga wiki iliyopita akiwa ndani ya kizuizi cha polisi nyumbani kwake, wimbo aliowaimbia polisi, wenye ujumbe kwamba hapigani na polisi, ila anawapigania kuboresha maisha yao na familia zao.

Bobi wine, amesomewa mashataka ya kutoheshimu majukumu ya serikali kinyume na ibara ya 116 ya sheria ya kanuni za adhabu, alipoongoza maandamanao katikati ya Jiji la Kampala, kupinga ushuru wa shilingi 200 kila siku kwa anayetumia mitandao ya kijamii ya Facebook, Whatsapp, Twitter, miongoni mwa mambo mengine.

Wadhamini wazuiliwa na polisi

Mawakili wake Bobi Wine, wakiongozwa na Katana Benjamin, wanasema polisi waliwazuilia wadhamini wake Bobi Wine kuingia mahakamani, wengi wao wakiwa wabunge, kumsimamia ili aweze kupewa dhamana.

"Kulikuwa na vizuizi vya polisi njia zote zinazoelekea mahakamani na waliokuja kumwekea dhamana walikamatwa na stakabadhi zote walizokuwa nazo kuchukuliwa na polisi. Hivyo hatungeweza kuwasilisha kwa jaji, karatasi za dhamana hiyo. Wamesema kuwa huku sio kutolewa haki, bali nihila za kisiasa," amesema.

Waandamanaji wafunga njia

Polisi walimzuilia kwa muda katika kituo cha polisi cha Nagalama, kilomita 50 mashariki mwa Kampala, lakini kufuatia maandamano ya vijana walioziba barabara wakitumia takataka na kuchoma matairi, polisi walimrejesha Kampala na kumfikisha mahakama ya Barabara ya Buganda.

Taarifa za mawakili wake zinasema kuwa alikuwa ametakiwa kufika ofisi ya upelelezi kujibu madai ya kuitisha maandamano baada ya polisi kumzuia kutumbuiza wafuasi wake sikukuu ya Pasaka.

Wafuasi wake kwenye mitandao ya kijamii wanaeleza kushutshwa kwao na hatua ya kufunguliwa kwake mashtaka kwa makosa ya mwaka 2018.

Wakili wa Bobi Wine Robert Amsterdam, kwa mara nyingine, amemwandikia barua Rais wa Marekani Donald Trump, akitaka Marekani kusitisha msaada wake kwa Uganda, akisema msaada wa silaha unaotolewa, unatumika na utawala wa Rais Yoweri Museveni kuwahangaisha raia wake. Bobi wine amepangiwa kurudishwa mahakamani Alhamisi saa nne asubuhi.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Kennes Bwire, Washington, DC.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG