Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 18:32

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi DRC kuanza mchakato wa kuorodhesha wapiga kura


Matayarisho ya kufunga vifaa vya uchaguzi yakiendelea kufanywa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi CENI. Picha kwa hisani ya CENI.
Matayarisho ya kufunga vifaa vya uchaguzi yakiendelea kufanywa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi CENI. Picha kwa hisani ya CENI.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, CENI  huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo  imethibitisha kuanza kwa mchakato wa kuorodhesha wapiga kura Jumamosi kwa ajili ya uchaguzi uliopangwa kufanyika Desemba 20, 2023. 

Uandikishaji wapiga kura utafanyika katika awamu tatu na kumalizika ifikapo Machi 17, 2023, yaani kila awamu itakuwa ni ya mwezi mmoja.

Awamu ya kwanza itahusisha majimbo kumi pamoja na majimbo ya Congo ya kati, Kinshasa, Kwango, Kwilu, Mai-Ndombe, Equateur, Mongala, Nord-Ubangi, Sud-Ubangi na Tshuapa.

Majimbo mengine yatafuatia baadae kabla ya kuanza kuorodhesha wapiga kura, CENI imezindua pia programu ya kidijitali iitwayo PRERAP inayoweza kupakuliwa kwa bure kutoka Internet Google appstore na google play, ambayo inaruhusu usajili wa haraka wa taarifa za mwombaji ili kupata kadi yake mpya ya mpiga kura kwa muda mfupi.

Programu hiyo, inaruhusu wapiga kura kujiandikisha mapema ili kupunguza muda wa kuwepo katika vituo vya kujiandikisha.

Kwa uchaguzi wa mwakani, CENI inakusudia kusajili wapiga kura zaidi ya milioni 50, wakiwemo wale wanaoishi katika nchi 5 za kigeni zilizochaguliwa katika awamu ya majaribio, ambazo ni Ufaransa, Marekani, Afrika Kusini, Canada na Ubelgiji.

Kiongozi wa tume ya taifa inayohusika na kuandaa uchaguzi Denis Kadima amesema CENI imeandaa mashine za kompyuta 30,000 pamoja na vifaa vingine muhimu kote nchini Congo ili kufanikisha operesheni hiyo kwa muda huo wa miezi mitatu.

Matayarisho ya kufunga vifaa vya uchaguzi yakiendelea kufanywa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi CENI. Picha kwa hisani ya CENI.
Matayarisho ya kufunga vifaa vya uchaguzi yakiendelea kufanywa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi CENI. Picha kwa hisani ya CENI.

Kiongozi anayehusika na mawasiliano kwenye tume hiyo Patricia Nseya Mulela, amesema zaidi ya vituo 29,000 vya usajili vitafanya kazi, yaani kumeongezwa vituo zaidi ya 12,000 vya usajili ikilinganishwa na marekebisho ya mwisho ya daftari la uchaguzi la mwaka 2016-2017.

Lakini ukiwa umesalia mwaka mmoja kabla kufanyika uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, hadi sasa bado kuna mashaka ya zoezi hilo kufanyika, kutokana na bajeti ya kufanikisha uchaguzi huo kama ilivyopangwa, masuala ya miundombinu ili vifaa vya uchaguzi vifikishwe katika vituo vya kupigia kura, na changamoto kubwa ya ukosefu wa usalama Mashariki ya Congo.

Licha yakuwa watu fulani-fulani (akina Matata Ponyo na Moise Katumbi) tayari wamejitangaza kuwa watagombea, inavyoonekana hadi sasa upinzani una mashaka, lakini mamlaka inazidi kuwapa moyo raia wake wahakikishe kuwa zoezi la uchaguzi linafanyika kama iliyopangwa.

Tume ya uchaguzi inaendelea kutoa uhakikisho kuhusu uendeshaji mzuri wa shughuli za uchaguzi katika maeneo ya Kwamouth katika jimbo la Mai-Ndombe na Bagata katika jimbo la Kwilu yaliyokumbwa na ghasia kufuatia mzozo wa kikabila kati ya Bateke na Bayaka.

CENI itahakikisha kwamba vifaa vya uorodheshaji vimewasili katika maeneo hayo yaliyokuwa na mizozo katika siku chache zijazo.

Makamu wa Mwenyekiti wa CENI Bienvenu Ilanga, amesema kuna kamati nzima inayo shughulikia suala la usalama ili kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unafanyika katika hali ya utulivu.

XS
SM
MD
LG