Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Septemba 19, 2024 Local time: 01:23

Mapambano makali kati ya ADF na wanajeshi baada ya waasi kuingia Uganda kutokea DRC


Wanajeshi wa Uganda wakiwa katika vita dhidi ya waasi wa ADF
Wanajeshi wa Uganda wakiwa katika vita dhidi ya waasi wa ADF

Mwanajeshi wa Uganda ameuawa katika mapambano na waasi wa kundi la Allied Democratic Forces ADF waliovuka mpaka kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kuingia katika wilaya ya Ntoroko, magharibi mwa Uganda.

Msemaji wa jeshi la Uganda Brig Felix Kulayigye amethibitisha kwamba mwanajeshi mmoja ameuawa pamoja na waasi 11.

Jeshi la Uganda limesema kwamba kundi la waasi karibu 30 lilivuka mto Semuliki na kuingia sehemu za wilaya za Kyanja na Ntoroko, kabla ya kukabiliwa na wanajeshi wa Uganda.

Waasi 8 wamekamatwa na bunduki 10 kupatikana.

Hii ni mara ya kwanza tangu miaka ya 1990 waasi wa ADF kuvuka mpaka na kuingia Uganda kutoka DRC.

Wanajeshi wa Uganda wanafanya operesheni maalum ndani ya DRC dhidi ya waasi wa ADF, ambao kamanda wao mkuu Jamil Mukulu anazuiliwa Uganda baada ya kukamatwa nchini Tanzania mwaka 2015.

Kundi hilo sasa linaongozwa na Musa Baluku. Inaripotiwa kwamba kundi hilo limegawanyika katika makundi mawili. kundi moja linaunga mkono Jamil Mukulu aliye gerezani na jingine linaongozwa na Baluku.

Wakati huo huo, muungano wa jeshi la DRC na Uganda umetangaza kuokoa raia 74 kutoka mikononi mwa kundi la ADF baada ya kuua waasi 30.

ADF ni kundi la waasi lililoanzia Uganda likipambana na utawala wa rais Yoweri Museveni, kabla ya kukimbilia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambako limejificha.

Limekuwa likitekeleza mashambulizi nchini Uganda na kukimbilia DRC.

Maafisa wa usalama wa Uganda wamelihusisha kundi la ADF na mauaji ya maafisa wa ngazi ya juu serikalini, wakiwemo maafisa wa polisi na jeshi.

ADF limehusishwa na mauaji ya mamia ya watu nchini DRC kila mwaka.

XS
SM
MD
LG