Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Juni 13, 2024 Local time: 14:36

DRC: Moise Katumbi kumenyana na Tshisekedi katika uchaguzi mkuu 2023


Mwanasiasa wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Moise Katumbi akizungumza na waandishi wa habari mjini Lubumbashi, Katanga, DRC, May 11, 2016
Mwanasiasa wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Moise Katumbi akizungumza na waandishi wa habari mjini Lubumbashi, Katanga, DRC, May 11, 2016

Mfanyabiashara maarufu, mwanasiasa na aliyekuwa gavana wa mkoa wa Katanga, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Moise Katumbi, ametangaza kwamba atagombea urais katika uchaguzi mkuu wa Desemba mwaka ujao 2023.

Katumbi, ambaye ni kiongozi wa chama cha Together for change yaani pamoja kwa ajili ya mabadiliko, alikuwa katika muungano mmoja wa kisiasa na rais wa sasa Felix Tshisekedi katika uchaguzi mkuu uliopita lakini anadai kwamba Tshisekedi ameshindwa kuiongoza nchi hiyo ya pili kwa ukubwa Afrika na yenye utajiri mkubwa wa madini.

Katika mahojiano na televisheni ya ufaransa, Katumbi amesema kwamba sababu yake kubwa ya kutaka kumuondoa Felix Tshisekedi madarakani katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao ni kutaka kusuluhsiha shida za Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na kulijenga jeshi la nchi hiyo.

Katumbi amesema kwamba ukosefu wa usalama mashariki mwa Congo unatokana na jeshi lisilokuwa na uwezo wa kupambana na adui, na kwamba jeshi hilo limedharauliwa ndani na nje ya nchi kwa miaka mingi.

Umaarufu wa Katumbi DRC

Katumbi anajulikana kote nchini Congo kutokana na uongozi wake wa mkoa wa Katanga wenye utajiri mkubwa wa madini, pamoja na kumiliki timu ya soka ya TP Mazembe.

Lakini wachambuzi na wasomi wa siasa za DRC kama Marcel Saila akiwa Canada, anasema kwamba Katumbi, namna alivyokabiliwa na vizuizi kadhaa katika uchaguzi mkuu uliopita alipotangaza kugombea urais, ndivyo atakavyokabiliana na vizuizi vivyo hivyo kwa mara nyingine, hasa utata unaohusu uraia wake.

“Kuna watu DRC wanasema kwamba Katumbi sio raia wa Congo wa kweli kwa sababu babake ni mzaliwa wa Ugiriki na mama yake ni raia wa Zambia. Wakati akiwa gavana, alisemekana kuwa na pasipoti ya Italy. Alipata pasipoti ya Congo baada ya Tshisekedi kuwa rais. Kulingana na katiba ya DRC, ikishaomba na ukapewa uraia wan chi nyingine, unapoteza uraia wa Congo. Kwa hivyo hilo litakuwa tatizo kubwa kwake.”

Uongozi wa katumbi katika mkoa wa Katanga kati ya mwaka 2007 na 2015 umesifiwa sana.

Katika uchaguzi wa mwaka 2018, aliungana na wanasiasa wengine kama Martin Fayulu, Felix Tshisekedi, Pierre Bemba, Vital Kamerhe, kabla ya muungano huo kuvunjika baada ya Fayulu kuchaguliwa kama mgombea kumenyana na Emmanuel Shadari wa chama kilichokuwa madarakani cha Democratic Republic of Congo.

Matokeo ya uchaguzi huo yalikumbwa na utata kabla ya tume ya uchaguzi kumuidhinisha Felix Tshisekedi kuwa mshindi, japo Martin Fayulu anadai kwamba alishinda uchaguzi huo.

Je, Katumbi ana sifa gani kujenga DRC?

Katumbi ni miongoni mwa watu tajiri sana nchini DRC na mwenye ushawishi mkubwa wa kisiasa na amekuwa na ushirikiano mzuri na rais wa sasa Felix Tshisekedi kiasi cha Tshisekedi kumpa paspoti ya DRC, iliyokuwa imefutwa na utawala wa Joseph Kabila.

“Hatuwezi kuchukua kazi ambayo alifanya Katanga na kuilinganisha na kusema anaweza kufanya vile vile kwa nchi kama DRC. Huduma zote kote Congo zimeharibika. Hakuna barabara, dawa kwa hospitali, yani huduma zote zimeharibika. Tukiangalia vile ameendesha hata hiyo timu ya mpira ya TP Mazembe ni kwa sababu alikuwa na pesa iliyomsaidia kulipa watu. Uhalisia wa nchi kama Congo sio hali ilivyo na timu ya mpira.” Amesema Marcel

Tshisekedi, ambaye aliingia madarakani kwa njia ya amani mwaka 2019 ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya DRC, aatarajiwa kugombea muhula wa pili.

Wagombea wengine wanaotarajiwa kwenye kinyang’anyiro cha urais ni pamoja na Augustin Matata Ponyo ambaye tayari ametangaza nia yake na Martin Fayulu.

Congo inakabiliwa na migogoro ya ndani hasa mapigano ya makundi ya waasi mashariki mwa nchi na tayari kuna wasiwasi kwamba huenda mazingira yakapelekea uchaguzi wa Decsmba 23, 2023 kuahirishwa.

Wapiga kura mashariki mwa DRC hawakushiriki upigaji kura wa mwaka 2018 kutokana na sababu za kiusalama.

XS
SM
MD
LG