Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Mei 22, 2024 Local time: 11:33

Putin avurumisha makombora ya masafa marefu 81 ndani ya Ukraine


Mtu anakimbia baada ya kombora la Russia kupiga gari mjini Kyiv. Oct. 10 2022
Mtu anakimbia baada ya kombora la Russia kupiga gari mjini Kyiv. Oct. 10 2022

Wanajeshi wa Russia wamerusha makombora katika miji kadhaa ya Ukraine wakati watu wakiwa wanaelekea kazini, na kuua raia, kuharibu mitambo ya umeme.

Rais Vladmir Putin ametangaza kwamba hatua hiyo ni ya kujibu shambulizi dhidi ya daraja linalounganisha Russia na Crimea.

Makombora yamepiga sehemu zenye shughuli nyingi za biashara, bustani na sehemu za kitalii mjini Kyiv.

Yamerushwa kwa kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa tangu wanajeshi wa Russia walipojaribu kuudhibithi mji mkuu wa Kyiv, mapema mwaka huu.

Milipuko imeripotiwa katika miji ya Lviv, Ternopil na Zhytomyr magharibi mwa Ukraine, Dnipro na Kremenchuk katikati mwa Ukraine, Zaporizhzhia kusini na Kharkiv mashariki mwa nchi hiyo.

Maafisa wa Ukraine wamesema kwamba watu 10 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa huku sehemu kubwa ya nchi ikibaki bila umeme.

Putin atishia kuendelea kurusha makombora ndani ya Ukraine

Katika hotuba kwa taifa, rais wa Russia Vladmir Putin amesema kwamba aliamuru mashambulizi hayo ya makombora ya masafa marefu dhidi ya mifumo ya nshati ya Ukraine.

Amesema pia kwamba makombora hayo yaliyorushwa kutoka angani, baharini na ardhini, yamelenga mifumo ya mawasiliano katika kile amekitaja kama kujibu mashambulizi ya kigaidi likiwemo shambulizi dhidi ya daraja la Kerch.

"Utawala wa Kyiv, kwa kuzingatia matendo yake, linafanana na makundi ya kimataifa ya kigaidi. Haiwezikani kukosa kuajibisha uhalifu kama huu. Asubuhi hii kwa kuzingatia ushauri wa waizara ya ulinzi na mpango wa jeshi la Russia, mashambulizi makubwa ya makombora ya masafa marefu ya angani, baharini na ardhini yamevurumishwa dhidi ya mfumo wa nshati wa Ukraine, kamand ya kijeshi na mawasiliano.” Amesema Putin.

Mpiganaji wa jimbo la Donetsk anayeungwa mkono na wanajeshi wa Russia.
Mpiganaji wa jimbo la Donetsk anayeungwa mkono na wanajeshi wa Russia.

Zelenskiy asema makombora yalilenga raia

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema kwamba mashambulizi ya makombora ya Russia yalilenga kuua raia wakati wanaelekea kazini, pamoja na kuharibu mfumo wa umeme.

Waziri mkuu wa Ukraine amesema kwamba mitambo 11 ya umeme imepigwa na kuharibiwa katika maeneo 8 ya nchi hiyo na kubaki bila umeme, maji au joto kwa ajili ya nyumbani.

"Ni asubuhi ngumu. Tunakabiliana na magaidi. Darzeni ya makombora ambayo yametengenezwa Iran yameharibu mfumo wa umeme kote nchini. Maeneo ya Kyiv na Khmelnytskyi, Lviv na Dnipro, Vinnytsia, Frankivsk, Zaporizhzhia, Sumy, Kharkiv , Zhytomyr, na Kirovohrad, kusini mwa nchi. Wanatafuta kuweka hali ya wasiwasi katika wat una kusababisha vurugu. Wanataka kuharibu mfumo wetu wa nshati. Wamepoteza matumaini. Shabaha yao ya pili ni watu. Waliamua kufanya uhalifu huo. Wameamua kufanya hivyo kwa wakati huo ili kusababisha uharibifu mkubwa wawezavyo lakini kama watu wa Ukraine, tunasaidiana. Tutarejesha kila kitu kilichoharibiwa. Kwa sasa, tutakuwa na ukosefu wa umeme kwa mda mfupi lakini umeme utarudi, ikiwa ni ishara ya ushindi,” amesema Zelenskiy.

Daraja liliharibiwa katika shambulizi la bomu

Shambulizi la mwishoni mwa wiki liliharibu daraja refu zaidi Ulaya, lililojengwa baada ya Russia kujiingiza Crimea mwaka 2014.

Ukraine inaliona daraja hilo kama njia inayotumiwa na Russia kuendelea na vita nchini Ukraine, na imefurahishwa na shambulizi hilo pasipo kudai kwamba imehusika na uharibifu wake.

Wanajeshi wa Russia wamekabiliwa na wakati mgumu katika vita vyao nchini Ukraine katika siku za hivi karibuni, huku vita hivyo vikikosolewa sana ndani ya Russia.

Umoja wa Ulaya wakemea makombora ya Russia

Daraja la Kerch linalounganisha Crimea na Russia lililoharibiwa Jumamosi Oct 8 2022
Daraja la Kerch linalounganisha Crimea na Russia lililoharibiwa Jumamosi Oct 8 2022

Ujerumani imesema kwamba jengo ambalo kuna ubalozi wake limepigwa katika mashambulizi ya makombora ya Russia.

Jengo hilo limekuwa halitumiki tangu vita vilipoanza Februari 24.

Umoja wa Ulaya umekemea vikali mashambulizi ya makombora ya Russia na kuyataja mashambulizi hayo ni “uoga”. Mataifa ya Magharibi vile vile yamekemea vikali mashambulizi hayo.

Wizara ya Ulinzi ya Ukraine imesema kwamba makombora 81 yamerushwa na Russia. Mfumo wa ulinzi wa Ukraine umepiga na kuharibu makombora 43.

XS
SM
MD
LG