Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 14:55

Pompeo atoa katazo dhidi ya maafisa kadhaa wa DRC kuingia Marekani


Mike Pompeo
Mike Pompeo

Marekani imesema Ijumaa kuwa iko pamoja na watu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kufuatia zoezi la kihistoria la kukabidhiana madaraka na kutangaza katazo la kuingia Marekani kwa maafisa kadhaa kutoka tume huru ya uchaguzi (INEC), serikali na jeshi la nchi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo anaweka wazi kwamba, kutokana na kujihusisha katika ufisadi mkubwa unaohusiana na mchakato wa uchaguzi, watu wafuatao: Corneille Nangaa, Mwenyekiti wa Tume huru ya uchaguzi (CENI) ya DRC, Norbert Basengezi Katintima, Makamu mwenyekiti wa CENI; Marcellin Mukolo Basengezi, Mshauri wa Mwenyekiti wa CENI; Aubin Minaku Ndjalandjoko, Spika wa Bunge la Taifa la DRC; na Benoit Lwamba Bindu, Rais wa Mahakama ya Katiba DRC, na familia zao za karibu hawataruhusiwa kuingia nchini Marekani.

Taarifa hiyo ya wizara imesema kuwa Kifungu 7031 cha Sheria ya Wizara ya Mambo ya Nje, operesheni za nje ya nchi imempa madaraka wakati wowote Waziri wa Mambo ya Nje akiwa na taarifa za uhakika kuwa maafisa wa serikali za kigeni wamejihusisha na ufisadi mkubwa au kuvunja kabisa haki za binadamu, watu hao na familia zao wasiruhusiwe kuingia Marekani.

Waziri huyo wa Mambo ya Nje pia ameweka katazo la viza kwa maafisa wa uchaguzi na maafisa wa serikali na jeshi ambao wanasadikiwa kuwa wamehusika kwa kusaidia, au kujihusisha na uvunjifu wa haki za binadamu au unyanyasaji au ukandamizaji wa mchakato wa demokrasia nchini DRC.

Taarifa hiyo ya wizara imesema kuwa watu hawa wamejitajirisha kupitia ufisadi, wameamrisha au kusimamia uvunjifu wa amani dhidi ya raia, wakati wananchi hao walipokuwa wanatekeleza haki zao za kukusanyika kwa amani na uhuru wa kujielezea. Walikuwa wanaendesha mambo bila ya kujali kwamba wanawaathiri wananchi wa Congo na wamekuwa wakionyesha waziwazi kutojali kwao misingi ya demokrasia na haki za binadamu.

Wizara ya Mambo ya Nje imesisitiza kuwa hatua hii iliyotangazwa leo inaelekezwa kwa maafisa maalum na siyo kwa wananchi wa Congo au serikali mpya iliyoingia madarakani.

Uamuzi huu unaonyesha nia ya Wizara ya Mambo ya Nje kuendelea kushirikiana na serikali mpya ya DRC katika kutekeleza ahadi zake za kutokomeza ufisadi na kuimarisha demokrasia na kuwajibika, na kuheshimu haki za binadamu.

Uchaguzi uliofanyika unaonyesha nia ya watu wa DRC kuleta mabadiliko na kuwa na taasisi za serikali zenye kuwajibika. Lakini hata hivyo kuna malalamiko ya kisheria juu ya mchakato wa uchaguzi jinsi ulivyoendeshwa na uwazi wake.

XS
SM
MD
LG