Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 01, 2022 Local time: 03:07

Mali : Upinzani wakataa mapendekezo ya Rais Keita


Rais Ibrahim Boubacar Keita

Rais Ibrahim Boubacar Keita wa Mali anakabiliwa na shinikizo la kuchukua uamuzi muhimu baada ya upinzani kukataa mapendekezo yake mapya. 

Akizungumza mwishoni mwa wiki ikiwa ni mara ya pili katika wiki moja, kiongozi huyo alisema anaivunja mahakama ya katiba kuitisha uchaguzi katika majimbo yaliokuwa na utata. Upinzani unashikilia lazima ajiuzulu.

Rais huyo anayefahamika zaidi kwa herufi za jina lake IBK, ameivunja mahakama ya katiba katika juhudi za kuzima malalamiko ya upinzani baada ya mahakama hiyo kufutilia mbali matokeo ya viti 30 vya bunge na kukipatia ushindi chama cha rais.

Rais IBK, aliahidi kuitisha tena uchaguzi katika wilaya hizo na kuanza mazungumzo ya kuunda serikali ya mpito.

Rais wa Mali amesema : “Napendelea mazungumzo na makundi yote ya taifa hili ili kuweza kuunda serikali ya maridhiano itakayo wakusanya pamoja wazalendo wa nchi na wala si waharibifu. Nitachukuwa hatua za kutekeleza mapendekezo ya jumuia ya uchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS.

Vuguvugu jipya la upinzani linaloongozwa na Imam wa jumuiya ya Kiislam mashuhuri Mahmoud Dicko na kuwaunganisha pamoja wanasiasa, wakuu wa dini na asasi za kiraia June M5-RFP, limepinga mapendekezo hayo.

Siku ya Jumapili Imam Dicko alitoa wito kwa wafuasi wao kutochochea ghasia baada ya watu 7 kuuliwa Ijumaa na Jumamosi wakati wa mapambano kati ya maafisa wa usalama na waandamanaji.

Mahmoud Dicko: “Kwa hakika ninawataka wasitumbukizwe kwenye mtego wa ghasia, kwa hakika tuna hitaji kuondoa ghasia katika vitendo vyetu. Dhamira yetu katika juhudi hizi ni kudumisha tena hadhi na heshima ya taifa la Mali.”

Maandamano ya upinzani yalianza Juni 5 mwezi uliopita na kufanyika kila Ijumaa yakimtaka rais Keita kuachia madaraka kwa kushindwa kutuliza mashambulizi ya wapiganaji wa Kiislamu kaskazini mwa nchi ambayo yameenea katika kanda ya Sahel tangu kuchukua madaraka 2013, pamoja na mapigano ya kikabila katikati ya nchi na madai ya utawala mbaya na ulaji rushwa ambao upinzani unasema umesababisha uchumi kudumaa.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG