Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 15:23

Kamala Harris awasili Ghana akiwa na msaada wa dola milioni 139


Mwanzilishi wa studio ya kurekodia kwa ajili ya wasanii chipukizi ya Vibrate Space iliyopo Accra, Sandy Alibo (katikati-kulia) akimkaribisha makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris alipoitembelea studio hiyo Machi 27, 2023. Picha na Nipah Dennis / AFP.
Mwanzilishi wa studio ya kurekodia kwa ajili ya wasanii chipukizi ya Vibrate Space iliyopo Accra, Sandy Alibo (katikati-kulia) akimkaribisha makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris alipoitembelea studio hiyo Machi 27, 2023. Picha na Nipah Dennis / AFP.

Makamu Rais wa Marekani Kamala Harris amekutana na Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo siku ya Jumatatu, akiwa amewasili na kitita cha dola milioni 139 ili kusaidia katika masuala ya usalama, uchumi na maendeleo kwa ajili ya nchi hizo mbili, ikiwa ni sehemu ya ziara hiyo ya mataifa matatu ya Afrika.

Ziara hiyo katika nchi za Ghana, Tanzania na Zambia itamalizika tarehe 2 Aprili, inafuatia mkutano wa kilele ulioandaliwa na rais Joe Biden mjini Washington mwezi Desemba na kuhudhuriwa na viongozi kutoka Afrika, ambapo Washington inatarajia kusawazisha ushawishi unaoongezeka wa China na Russia barani Afrika.

"Tunatarajia kuitumia ziara yako hii kama chanzo wa kufufua na kupanua mahusiano haya," kiongozi huyo wa Ghana alisema.

Siku na Jumanne makamu wa rais Harris atazungumza katika Kasri la Cape Coast, mahali ambako watumwa wa kiafrika walipandishwa meli zilizoelekea Marekani, kipindi kilichoweka dosari ya kihistoria kwa nchi zote mbili.

Siku ya Jumatano, makamu wa rais atakutana na wafanyabiashara wanawake, wakati mume wake akitembelea kiwanda cha kutengeneza chokoleti kilichoanzishwa na madada wawili.

Ikipambana na misukosuko ya kiuchumi, deni linaloongezeka na mfumuko wa bei wa zaidi ya asilimia 50, Ghana imekubali kupokea mkopo wa dola bilioni tatu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Katika taarifa ya awali, ofisi ya Harris ilisema utawala wa rais Biden utawekeza dola milioni 100 kama sehemu ya mpango wa kuzisaidia Ghana, Benin, Togo na Ivory Coast katika kuleta utulivu na kukabiliana na tishio la jihadi.

Washington itatuma mshauri maalum nchini Ghana kuisaidia serikali ya Akufo-Addo na wasifu wake wa deni mwaka huu.

Baada ya Ghana, atasafiri Jumatano kwenda Dar es Salaam nchini Tanzania.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP

XS
SM
MD
LG