Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 20, 2024 Local time: 15:53

Tanzania imekopa tena dola bilioni 2.2 licha ya ukosoaji mkali wa raia wake


Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alipohudhuria mazishi ya aliyekuwa rais wa nchi hiyi hayati John Magufuli katika uwanja wa michezo wa Chato, Tanzania, March 26, 2021.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alipohudhuria mazishi ya aliyekuwa rais wa nchi hiyi hayati John Magufuli katika uwanja wa michezo wa Chato, Tanzania, March 26, 2021.

Serikali ya Tanzania imetangaza kupokea mkopo wa dola bilioni 2.2 kutoka China ili kusaidia kukamilisha ujenzi wa reli ya mwendo wa wastani SGR.

Makubaliano hayo na kampuni za China za CCECC na CRCC, yatapelekea ujenzi wa sehemu ya reli iliyosalia, kilomita 506 kutoka Tabora hadi Kigoma na kazi hiyo imepangiwa kukamilika mwaka 2026.

Ujenzi wa reli ya SGR kutoka bandari ya Dar-es-salaam hadi Mwanza utaweka nafasi nzuri ya reli hiyo kuunganisha Burundi, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Rwanda na Uganda.

Haya yanajiri wakati kuna mjadala mkubwa nchini Tanzania kuhusu kuongezeka kwa deni la taifa na kufikia Trilioni 91 huku serikali ikiendelea kukopa.

Usiri mkubwa ulizunguka namna serikali ya Tanzania ilivyokuwa ikifadhili miradi yake ya maendeleo wakati wa utawala wa Hayati John Magufuli.

‘Mikataba ya kijinga na mwendawazimu’

Magufuli alisisitiza kwamba miradhi kadhaa ilikuwa inatekelezwa kwa pesa za serikali.

Alikuwa na msimamo mkali dhidi ya mikopo kiasi kwamba alifuta mojawapo ya mradi mkubwa wa ujenzi wa bandari, akitaja mkataba uliokuwa umeandikwa kuwa mkataba wa kijinga ambao unaweza tu kukubaliwa na mwendawazimu.

Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye alikuwa makam wa Magufuli, amekosolewa sana kwa kukopa, kiasi cha kutokea mvutano ndani ya chama cha mapinduzi CCM, kinachotawala Tanzania.

Aliyekuwa Spika Job Ndugai alilazimika kujiuzulu baada ya kukosoa hadharani utawala wa rais Suluhu Hassan, akisema kwamba nchi ilikuwa inapigwa mnada kwa kuongeza kukopa kila mara.

Mjadala mkubwa Tanzania ni kwamba nchi inakopa lakini mabadiliko ya kiuchumi katika Maisha ya raia wa Tanzania hayaoenikani.

Msomi wa maswala ya uchumi Tanzania Walter Nguma anasema serikali kukopa kwa ajili ya maendeleo ni hatua nzuri lakini serikali inastahili kujibu maswali yanayoulizwa na watanzania.

“Tunaambiwa sasa deni la taifa limefika shilingi za Tanzania trilioni 91. Hapa lazima watu waulizane kuhusu usiziri unaozunguka ukopeshaji wenyewe. Ni mikopo ambayo inachukuliwa kwa ajili ya miradi ambayo tayari ilianzishwa. Sasa swali ni kwamba kama miradi ilianzishwa, na kuna mikopo iliyochukuliwa awali, mkopo unaochukuliwa kwa ajili ya mradi ulioanza ni wa nini, ni wa namna gani? Na zile pesa zilizochukuliwa awali zilifanya kazi kwa kiasi gani na kiwango gani? Ufafanuzi umekuwa mdogo sana,” amesema Nguma.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na mwenyeji wake Rais wa China Xi JInping. China ni mkopeshaji mkubwa wa nchi za Afrika. Picha kwa hisani ya Ikulu ya Dar es Salaam.
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na mwenyeji wake Rais wa China Xi JInping. China ni mkopeshaji mkubwa wa nchi za Afrika. Picha kwa hisani ya Ikulu ya Dar es Salaam.

Tanzania imekopa kutoka benki ya Dunia, IMF na ADB mwaka 2022

Miongoni mwa mikopo ambayo Tanzania imekopa miezi ya hivi karibuni ni pamoja na dola bilioni 1.05 kutoka kwa shirika la fedha la kimataifa IMF kwa ajili ya kukabiliana na athari za vita vinavyoendelea nchini Ukraine na janga la virusi vya Corona. Mkopo huo ulitolewa mwezi July mwaka huu.

Kabla ya mkopo huo, IMF lilikuwa limetoa mkopo wa dola milioni 90.6 kwa Tanzania kwa ajili ya kilimo na huduma za kifedha vijijini kwa lengo kubwa la kukabiliana na umaskini.

Mkopo wa dola milioni 125.2 kukabiliana na uhaba wa maji katika wilaya tatu za Bahi, Chemba na Chamwino, eneo la Dodoma, ambao ulitolewa na benki ya maendeleo Afrika. Mkopo huo ulichukuliwa kwa ujenzi wa bwawa la maji la Farkwa.

Mwaka huu vile vile, Tanzania imekopa dola milioni 650 kutoka kwa benki ya dunia kwa ajili ya miradi ya elimu.

Hii ina maana kwamba mwaka huu 2022, Tanzania imekopa kutoka kwa mashirika makubwa yote yanayotoka mikopo, ambayo ni benki ya Dunia, IMF, na benki ya maendeleo Afrika.

Mikopo kutoka China na nchi zingine

Yapo makubaliano ya kifedha na ya mikopo kati ya nchi kwa nchi, ambayo taarifa za undani kuihusu imesalia kuwa siri kwa kiasi Fulani.

Rais Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kwamba serikali itaendelea kukopa kwa ajili ya kuimarisha maendeleo nchini na wala hakuna haja ya raia wa Tanzania kuwa na hofu kuhusu mikopo anayochukua na kwamba nchi ina uwezo wa kulipa madeni yake.

Wizara ya fedha na benki kuu ya Tanzania, wamesisitiza kwamba madeni ya nchi ni nafuu.

Ripoti ya benki kuu ya Tanzania ya mwezi Novemba inasema kwamba deni la Tanzania limefikia dola milioni 39,006.1 na linaongezeka kwa dola milioni 544.8 kila mwezi.

Kufikia mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu 2022, asilimia 70.5 ya deni la serikali ni kutoka kwa wakopeshaji wa nje, huku wakopeshaji wa ndani wanadai serikali shilingi trilioni 26.6, pesa za Tanzania.

Tanzania miongoni mwa nchi 34 Afrika zenye madeni mengi

Kulingana na Benki ya dunia, pamoja na shirika la fedha ulimwenguni, Tanzania ni miongoni mwa nchi 34 za Afrika zenye kiwango kikubwa cha madeni.

Nchi zingine ni Ghana, Ethiopia, Benin, Burundi, Cameroon, Afrika ya kati, visiwa vya Comoros, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Rwanda, Somalia, Sudan, Uganda, Togo, Zambia miongoni mwa nyingine.

Kitunda Nassor, mhadhiri wa saikolojia, jamii na maendeleo katika chuo kikuu cha Dar-es-salaam, anasema kwamba Tanzania imekuwa ikikopa kwa muda mrefu na wala hilo halijaanza na rais Samia Suluhu Hassan. Nassor, ana mtazamo kwamba baadhi ya mikopo, inatumika kama diplomasia ya mikopo, ambayo ni sawa na mtego.

Wakosoaji wa serikali ya Tanzania, kwa kiwango Fulani wanakubaliana kwamba ni vigumu kwa nchi inayoendelea kwama Tanzania kukosa kukopa lakini ikifika kiasi kwamba asilimia 60 ya mapato ya nchi inatumika kulipa deni, basi kuna shida kubwa kwa taifa.

Wanasisitiza kwamba mikopo inastahili kutumika kuimarisha sekta za uzalishaji na kwa haraka ili nchi iwe huru na mikopo na isigeuke kuonekana kama mnada.

Wataalam wa uchumi wanataka serikali kuwezesha bunge kuwa na uwezo wa kuamua mikopo ambayo serikali inaweza kuchukua na ile isiyofaa.

XS
SM
MD
LG