Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Aprili 02, 2023 Local time: 14:37

Rais Paul Kagame auzungumzia mzozo wa DRC


kagame-rwanda

Rais Paul Kagame wa Rwanda kwa mara nyingine tena amekwenda mbali na kuzungumzia mzozo unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kati ya wanajeshi wa serikali na wapiganaji wa kundi la M23.

Kundi hili tayari limekwisha kamata maeneo mengi mashariki mwa nchi hiyo.
Katika siku za hivi karibu wakati mzozo huu ukishika kasi viongozi mjini Kinshasa mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kigali mji mkuu wa Rwanda wanaendelea kurushiana cheche za maneno.
Akiwapokea kwenye dhifa maalum wanadiplomasia wakiwemo mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa,
Rais huyo wa Rwanda amesema hali inayoshuhudiwa kwa sasa nchini DRC ilikuwepo zaidi miongo miwili iliyopita .
" Ngoja niwape mfano, matatizo ya kile kinachotokea kati na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,au kinachotokea mashariki mwa nchi hiyo, kimekuwepo kwa zaidi ya miaka 25 sasa, na mambo yanaendelea kutokea aghalabu kila baada ya miaka mitano, sawa na haya mnayoyaona sasa. Kama ambavyo nimeeleza kinachotokea sasa, kilitokea mwaka 2012" Kagame amesema
Mchango wa jumuiya ya kimataifa
Akizungumzia jumuiya ya kimataifa kwenye mzozo wa DRC Rais Paul Kagame ameilaumu jumuiya ya kimataifa kuufumbia macho mzozo huo kutokana na maslahi ya kisiasa huku akibaini kwamba kuendelea kupuuzia kiini cha mzozo kunakofanywa na jumuiya hiyo hakutatui matatizo isipokuwa yanaufanya mzozo huo kuwa mgumu zaidi.
Kagame amesema kwamba haelewi ni kwa nini diplomasia na siasa kwenye ulimwengu wa leo vinapuuza ushahidi kuhusu athari za matatizo yanayoonekana wazi na kuamua kila kitu kukifanya ni siasa.
"Hebu fikiria tumekuwa na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa - MONUSCO karibu miaka 20 sasa,na nimekuwa najiuliza ikiwa siasa na diplomasia havina matatizo kama nilivyosema, kwa nini uendelee kuwa na maelfu ya wanajeshi wa kulinda amani katika eneo ambalo kwa zaidi ya miaka 20 kwa gharama ya mabilioni ya dola na hali inaendelea kuwa hivi siku zote," Rais Kagame alihoji.
Kikosi cha kulinda amani nchini DRC MONUSCO chenye wanajeshi zaidi ya elfu 12 hutumia bajeti ya dola bilioni moja kila mwaka,lakini Rais Paul Kagame anasema inaonekana Jumuiya ya kimataifa inaridhika na kazi inayofanywa na MONUSCO.
Katika hotuba yake kwa wanadiplomasia wakiwemo mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa Rais Kagame amewalaumu viongozi wa DRC akiwemo Rais wa nchi hiyo Felix Tsishekedi ambaye ameshindwa kutatua changamoto zinazoikabili nchi yake na badala yake anaamua kulikimbia tatizo kwa kulilibebesha majirani zake kama Rwanda.
Kagame amesema kwamba viongozi mjini Kinshasa akiwemo Rais Tsishekedi wamekuwa na lugha zinazopotosha hali ambayo inaufanya mzozo huu kushindwa kupata suluhu.
Rais Kagame amefafanua jinsi viongozi wa DRC walivyoupotosha ulimwengu baada ya kikao cha dharura cha viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika mjini Bujumbura nchini Burundi wiki iliyopita tarehe 4 Februari 2023.
" Juzi tulikuwa mjini Bujumbura, alikuwepo Rais wa DRC na ujumbe wake tulizungumzia matatizo haya kwa mapana na kwa uwazi na yeye alishiriki ,na baadaye tukaandika tangazo la pamoja ili kuufahamisha umma kile tulichokizungumzia na mstakabali wake, tangazo likasomwa lakini siku ya pili, tangazo jingine lenye ujumbe kinyume na haya likasomwa Kinshasa" alisema Rais wa Rwanda.
FDLR mzizi wa Fitina
Rais Paul Kagame amewalaumu watalaam wa Umoja wa Mataifa ambao siku zote wamekuwa wakifanya uchunguzi wa kashfa inayoendelea kulikumba eneo la mashariki mwa DRC, bila kufafanua kinagaubaga uwepo wa kundi la wapiganaji wa kihutu la FDLR ambao Rwanda inaendelea kulibebesha jukumu la kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya watutsi wa Rwanda 1994.
Kagame amehoji kwa nini kwenye ripoti wachunguzi wa Umoja wa Mataifa hawafafanui wazi jinsi kundi linavyoendelea kueneza itikadi ya chuki kufanya mauaji ya raia wa DRC wanaodhaniwa kuwa na chimbuko kutoka Rwanda.
Hata hivyo ameionya jumuiya ya kimataifa kwa kutumia lugha ya mafumbo akisema badala ya kuilaumu Rwanda kujiingiza kwenye mzozo wa DRC kwa nini wasijiulize kwa nini Rwanda ingefanya hivi?
Rwanda inailaumu DRC kuwa uungaji mkono wapiganaji wa FDLR kwa kushirikiana na jeshi la serikali ya DRC huku serikali ya Congo ikiilaumu Rwanda kujiingiza kwenye mzozo wa DRC kwa kuwaunga mkono waasi wa M23.
Imetayarishwa na mwandishi wetu Slyivanus Karemera, Rwanda

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG