Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Mei 27, 2024 Local time: 03:59

Papa Francis: Acheni kupora mali ya DRC! Ondoeni mikono yenu DRC!


Papa Francis (kushoto) akiwa na rais wa DRC Felix Tshisekedi alipowasili Kinshasa Januari 31, 2023
Papa Francis (kushoto) akiwa na rais wa DRC Felix Tshisekedi alipowasili Kinshasa Januari 31, 2023

Kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Francis, ameyataka mataifa ya nje kuacha kupora mali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na bara la Afrika kwa jumla, ili kutosheleza tamaa yao.

“Ondoeni mikono yenu DRC! Ondoeni mikono yenu Afrika!” amesema Papa Francis wakati anaanza hotuba yake mbele ya maafisa wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wanadiplomasia na viongozi mbalimbali wa DRC, katika ikulu ya rais mjini Kinshasa.

Francis amehubiri amani na upendo katika hotuba yake ya kwanza alipofika Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo leo Jumanne.

Ziara ya papa DRC inajiri wakati serikali ya rais Felix Tshisekedi inakabiliana na mashambulizi kutoka kwa mamia ya makundi ya waasi mashariki mwa nchi hiyo.

Papa Francis ameeleza masikitiko kwamba hataweza kufika katika mji wa Goma kutokana na ghasia zinazoendelea sehemu hiyo.

Papa Francis atakuwa DRC kuanzia leo (Jumanne 31 Januari 2023) hadi Februari 3.

Francis anakuwa kiongozi wa pili wa kanisa katoliki kutembelea DRC, baada ya papa mtakatifu John Paul II aliyeitembelea nchi hiyo mwaka 1980 na 1985.

Ziara ya Papa Francis nchini DRC na Sudan Kusini, ni ziara yake ya 5 barani Afrika.

Aliitembelea Kenya, Uganda na Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 2015. Alirudi tena Afrika mwaka 2017 alipoitembelea Misri na baadaye mwaka 2019 alipokwenda Morocco, Msumbiji, Madagascar na Mauritius.

Ziara yake DRC na Sudan Kusini, ilipangwa ufanyika mwaka 2022 kabla ya kuahirishwa kutokana na maumivu ya goti.

Asilimia 20 ya wamumini wa kanisa Katoliki wako Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na idadi ya waumini inaendelea kuongezeka.

Utajiri mkubwa DRC lakini mizozo imeshamiri

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ina utajiri mkubwa wa madini yenye thamani kubwa zaidi duniani ikiwemo almasi, dhahabu, shaba, cobalt, tentalum na lithium lakini vita kati ya makundi ya waasi na wanajeshi wa serikali pamoja na uvamizi wa nchi Jirani vimepelekea raia wa DRC kuishi katika umaskini mkubwa.

Mapigano yanaendelea DRC kati ya kundi la waasi la M23 na wanajeshi wa DRC, na yanahusiana na mauaji ya kimbari yaliyotokea katika nchi Jirani ya Rwanda mwaka 1994, serikali ya Rwanda ikishutumu DRC kwa kuunga mkono waasi wa FDLR.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu milioni 5.7 wanakabiliwa na uhaba wa chakula nchini Congo.

Kanisa katoliki linajihusisha na maendeleo ya kila aina nchini DRC, ikiwemo elimu, mfumo wa afya na demokrasia.

XS
SM
MD
LG