Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Mei 18, 2024 Local time: 17:33

Wasifu wa Samia Suluhu Hassan : Rais wa kwanza mwanamke Tanzania


Samia Suluhu Hassan
Samia Suluhu Hassan

Samia Suluhu Hassan anakuwa rais wa kwanza mwanamke nchini Tanzania. Samia anashika wadhifa huo baada ya kuhudumu kama Makamu Rais na kwa mujibu wa katiba, kufuatia kifo cha Rais Magufuli anatakiwa kisheria kushika wadhifa wa urais.

Samia Suluhu mwanasiasa wa chama tawala cha CCM alizaliwa Zanzibar Januari 27, mwaka 1960. Aliianza safari yake ya kisiasa mwaka 2000 alipochaguliwa katika baraza la wawakilishi la Zanzibar kama mwakilishi wa kiti maalum na kuteuliwa na kushika wadhifa wa uwaziri na Rais wa Zanzibar wakati huo, Amani Karume, akiwa mwanamke pekee katika nafasi ya juu ya uwaziri katika baraza hilo la mawaziri.

Mwaka 2010 Bi Samia akaona ni vyema kuwania ubunge katika bunge la Jamhuri ya muungano ambapo alishinda kiti cha jimbo la Makunduchi kwa kupata takriban asilimia 80 ya kura.

Safari yake katika uongozi wa serikali ilianzia pale ambapo alichaguliwa na Rais Jakaya Kikwete mwaka 2014 kuwa waziri wa nchi katika masuala ya muungano. Wakati Tanzania ilipokuwa katika mchakato wa kujadili katiba mpya ya nchi alichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa bunge la katiba na kushiriki jukumu muhimu la kuandika rasimu ya katiba mpya.

Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete

Samia alisoma katika shule za Ng’ambo na Lumumba mjini Unguja, baadaye alijiunga na Taasisi ya Utawala wa Fedha ZIFA kwa masomo ya takwimu. Baada ya masomo hayo aliajiriwa katika wizara ya mipango na maendeleo na baadaye kujiunga na Chuo kikuu cha Mzumbe mkoani Morogoro. Alihudhuria pia masomo ya juu katika chuo kikuu cha Manchester huko London, Uingereza na kupata shahada ya uchumi na pia amesoma katika chuo kikuu cha New Hampshire hapa Marekani.

Samia ni Makamu Rais wa kumi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alishika wadhifa huu mara ya kwanza November 5, mwaka 2015, chini ya Rais John Magufuli.

Makamu Rais Samia Suluhu (kushoto) na hayati Rais John Magufuli
Makamu Rais Samia Suluhu (kushoto) na hayati Rais John Magufuli

Mwaka 2015 gazeti la Mshale liliandika kuhusu kupanda katika nyanja ya siasa za Tanzania kwa Bi Samia na kuuliza swali, “je mwanamke anaweza kupanda na kuwa rais katika nchi yoyote ya Afrika Mashariki? Tusubiri tuone muda tutapata jibu gani.” Leo hii bi Samia anatoa jibu kwa kushika wadhifa wa rais na kuwa mwanamke wa kwanza katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Samia aliolewa na Hafidh Ameir mwaka 1978, na kujaaliwa watoto wanne mmoja wa kike na watatu wa kiume. Ni mtoto wake wa kike Mwanu Hafidh Ameir ndiye aliyefuata nyayo za mama yake na kuwa mwakilishi katika baraza la wawakilishi Zanzibar.

XS
SM
MD
LG