Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Novemba 30, 2022 Local time: 14:00

Rais Magufuli afariki dunia


Rais John Pombe Magufuli

Rais Magufuli alichaguliwa kuiongoza Tanzania kwa mara ya kwanza mwaka 2015 na Oktoba, 2020 alichaguliwa kushika awamu ya pili ya miaka mitano. Kulingana na katiba ya Tanzania Makamu Rais Samia Suluhu Hassan atamalizia muhula huo.

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amefariki dunia siku ya Jumatano jioni baada ya kuugua kwa muda mfupi. Alikuwa na umri wa miaka 61. Kifo cha Rais Magufuli kimetangazwa katika televisheni ya taifa TBC na Makamu Rais Samia Suluhu Hassan majira ya saa tano na nusu kwa saa za Dar es salaam.

Kulingana na tangazo la Makamu Rais Hassan kiongozi huyo wa Tanzania kwa kipindi cha miaka sita iliyopita alifariki majira ya saa kumi na mbili jioni katika hospitali ya Mzena mjini Dar es salaam kutokana na matatizo ya moyo. Hassan alisema marehemu Magufuli alianza kuugua tarehe March 6 na kulazwa katika hospitali ya Muhimbili na baadaye kuhamishiwa katika hospitali ya Mzena.

Kifo cha Magufuli kimekuja wiki tatu baada ya kiongozi huyo kutoonekana hadharani na kuzusha uvumi ulionea ndani na nje ya kwamba anaumwa na amepelekwa nje ya nchi kwa matibabu.

Rais Magufuli atakumbukwa kwa mengi hasa juhudi alizofanya katika kuleta maendeleo Tanzania katika muda mfupi wa utawala wake. Lakini pia atakumbukwa katika siku hizi za mwisho za maisha yake kwa msimamo mkali kuhusu janga la Covid 19 ambalo limeutikisa ulimwengu kwa kusema Tanzania imefanikiwa kutokomeza virusi vya corona kwa sala na kutumia dawa za miti shamba na hivyo kuwataka wananchi wasiwe na khofu kamwe Covid haitaliyumbisha taifa.

Kulingana na katiba ya Tanzania Makamu Rais Samia Hassan atachukua uongozi wa nchi hiyo. Lakini hadi sasa haijatangazwa kama ameshaapishwa au lini ataapishwa.

Tanzania bado haijatangaza ratiba ya maziko, lakini kuanzia Jumatano usiku bendera zimekuwa zikipepea nusu mlingoti.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG