Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 20, 2024 Local time: 15:12

COVID-19 : Majaliwa awataka Watanzania kuomba Mungu na kuwasikiliza wataalam


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.(Picha kwa hisani ya Michuzi Blog)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.(Picha kwa hisani ya Michuzi Blog)

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Watanzania wanaweza kuushinda ugonjwa wa corona kwa kumuomba Mungu na kufuata ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya kuhusu njia za kujikinga na ugonjwa huo.

“Katika kipindi hiki ambacho dunia imekumbwa na wimbi la ugonjwa wa mlipuko, muhimu sisi kuendelea kumuomba Mungu kama Mheshimiwa Rais alivyotuasa tufunge na tufanye maombi ya siku tatu; Ijumaa kwa Waislamu kama walivyofanya, Jumamosi kwa Wasabato tumeona mwitikio wao na kwa Wakristo kesho Jumapili kama tulivyoona maandalizi yakifanyika,” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Rais John Pombe Magufuli katika mazishi ya aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, leo (Jumamosi, Februari 20, 2021) Waziri Mkuu amesema: “Pamoja na kumuomba Mungu, ni lazima tuendelee kufuata maelekezo ya kitaalam ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka, tutumie vitakasa mikono na kuvaa barakoa.”

Kuhusu uvaaji wa barakoa, Waziri Mkuu amesema Serikali haijazuia mtu kujikinga lakini aliwataka wanaozitumia ni lazima wajiridhishe na ubora, usalama wake na wafahamu zimetoka wapi. “Ni lazima wanaozitumia wajue zimetoka wapi. Ni vema watu washone barakoa zao wenyewe au wanunue zilizotengenezwa na viwanda vya Tanzania kama alivyoshauri Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli mwaka jana.”

Amesema: “Pamoja na maombi, Watanzania tunapaswa tuendelee kufuata maelekezo ya Serikali bila kuwa na hofu. Serikali kupitia maabara na vituo vya kutoa huduma, inaendelea kuhakikisha huduma zinapatikana.

Akimzungumzia marehemu Balozi Kijazi, Waziri Mkuu aliwapa pole wafiwa na wanafamilia kutokana na msiba huo mkubwa na alimuelezea kwamba, alikuwa kiongozi mwenye mapenzi mema na Taifa lake lakini pia alikuwa na uwezo wa kutoa ushauri ambao ulikuwa na manufaa kwa Taifa. “Tunalo jukumu la kumuenzi kwa kuendeleza na kutenda mema yote aliyotuachia.”

Gari ilioubeba mwili wa Balozi John Kijazi
Gari ilioubeba mwili wa Balozi John Kijazi

Ibada ya kumuombea Marehemu Balozi Kijazi ilifanyika katika kanisa la Mt. Agustino, eneo la Manundu, mjini Korogwe, mkoani Tanga na iliongozwa na Askofu Mstaafu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, Mhashamu Telesphory Mkude.

Mapema, akizungumza katika mazishi hayo, Mkuu wa Majeshi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo alisema wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama walikuwa karibu naye kwa sababu Balozi Kijazi alikuwa ni Katibu wa Baraza la Usalama la Taifa.

“Alikuwa ni mahiri, mpole na mwenye uwezo mkubwa wa kujenga hoja ambazo zilieleweka na kukubalika katika vikao vyao,” alisema.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bw. Martine Shigela alisema Balozi Kijazi alikuwa ni Baba, kiongozi na mwalimu na wakati wote alikuwa ni kielelezo cha uchapakazi na uadilifu kwa watu wa mkoa wa Tanga. “Na kwa sababu hiyo, mkoa umeamua kuwa stendi ya mabasi ya mji wa Korogwe itapewa jina la Balozi John Kijazi kwa heshima yake ili kutunza kumbukumbu yake,” aliongeza.

Mazishi hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu na Wabunge wa mkoa wa Tanga.

Mhandisi Balozi Kijazi alizaliwa mkoani Mwanza akiwa ni mtoto wa pili kwenye familia ya watoto 10. Ameacha mke, watoto watatu pamoja na wajukuu wawili.

XS
SM
MD
LG