Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Mei 01, 2024 Local time: 07:59

Kutoonekana kwa Magufuli kwazua wasiwasi kuhusu afya yake


Rais John Magufuli
Rais John Magufuli

Ripoti za mitandaoni na matamshi ya viongozi wa upinzani nchini Tanzania pamoja na kutoonekana hadharani kwa Rais John Pombe Magufuli kwa zaidi ya wiki moja sasa kumezusha wasiwasi kuhusu afya yake, huku kukiwa na ripoti zisizo thibitishwa na vyombo rasmi kwamba amelazwa katika hospitali moja mjini Narobi, Kenya, tangu Jumatatu wiki hii.

Shirika la habari la Reuters limemkariri kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, ambaye anaishi uhamishoni nchini Ubelgiji akiitaka serikali ya Tanzania kutoa habari kuhusu afya ya Rais Magufuli kufuatia uvumi kuwa huenda anapatiwa matibabu nje ya nchi.

Tundu Lissu
Tundu Lissu

Mitandao ya kijamii na upinzani nchini Tanzania inadai kuwa Magufuli, ambaye amepata umaarufu mkubwa barani Afrika kwa kudai kuwa nchi yake haina janga la Covid-19 anashukiwa huenda ameambukizwa virusi vya Corona, lakini hakuna uthibitisho wowote rasmi uliotolewa na serikali.

Gazeti la The Nation la Kenya limekariri vyanzo vya kisiasa na kidiplomasia vikisema kuwa “kiongozi wa nchi moja ya Afrika ambaye hajaonekana hadharani kwa takriban wiki mbili” amewekwa katika mashine ya kupumulia katika hospitali moja ya mjini Nairobi akisadikiwa kuwa anaugua Covid-19.

Magufuli mwenye umri wa miaka 61, ambaye amepewa jina la utani ‘Bulldozer’ mara ya mwisho alionekana hadharani Februari 27, akionekana yuko katika hali ya kawaida alipomuapisha Waziri Kiongozi huko Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Reuters, mkurugenzi wa mawasiliano Gerson Msigwa na msemaji wa serikali Hassan Abbas hawakujibu ujumbe wa shirika hilo ili watoe maoni kuhusu uvumi unaoendelea. Mwakilishi wa wizara ya mambo ya nje ya Kenya naye hakupatikana kuelezea habari hizo na Hospitali ya Nairobi nayo haikutoa habari zozote walipoulizwa na Reuters.

“Afya ya rais ni jambo ambalo linatia wasi wasi kwa umma. Magufuli ana kitu gani ambacho sisi hatustahili kufahamu,” Kiongozi wa upinzani Tundu Lissu amesema katika Tweet yake Jumanne jioni huku uvumi ukisambaa kwenye mitandao ya kijamii nchini Tanzania.

“Ni jambo la kusikitisha kwa upande wake kwa nchi yetu kwamba imefikia hali hii: Rais mwenyewe amepata Covid 19 na kupelekwa nchini Kenya, hii inathibitisha kwamba sala, kujifukiza na dawa za miti shamba ambazo amekuwa akizipigia debe hazina ulinzi wowote dhidi ya virusi vya corona,” ameongezea Lissu, amesema bila ya kutoa ushahidi.

Magufuli ana historia ya matatizo ya moyo, kwa mujibu wa daktari mmoja mwandamizi nchini Tanzania ambaye yuko karibu na serikali ameomba asitajwe jina, na afisa wa usalama nchini Kenya mwenye mawasiliano na serikali nchini Tanzania.

Chanjo Si Nzuri’

Magufuli amepuuza tishio la Covid-19 nchini Tanzania na kubeza taharuki ambayo imejitokeza kote ulimwenguni. Amewasihi Watanzania kuweka imani yao katika sala na tiba mbadala za dawa za miti shamba kama vile kujifukiza badala ya chanjo, ambazo amesema ni hatari sana na sehemu ya njama za Magharibi.

Chanjo ya Covid-19 ya kampuni ya Johnson & Johnson
Chanjo ya Covid-19 ya kampuni ya Johnson & Johnson

“Chanjo si nzuri. Kama zilikuwa nzuri basi wazungu wangekuwa wameshapata chanjo ya HIV/Ukimwi,” alisema mapema mwaka huu.

Tanzania iliacha kuripoti kuhusu data za virusi vya corona nchini humo tangu Mei mwaka 2020 wakati mara ya mwisho iliripoti kuwa kulikuwa na kesi 509 na vifo 21, kwa mujibu wa data zaz Shirika la Afya Duniani (WHO).

Hata wakati Covid-19 ikiwa inasambaa kote Afrika, Watanzania bado wanaruhusiwa kukusanyika pamoja, kwa mfano kwenda kuangalia michezo. Rais alibeza vifaa vya kupima virusi ambavyo viliagizwa kutoka nje, akisema vifaa hivyo pia viliweza kubainisha kuwa mbuzi na mapapai yalikuwa ya virusi vya corona.

Magufuli alichaguliwa mara ya kwanza kuongoza Tanzania, mwaka 2015. Mwaka jana alichaguliwa tena baada ya kumshinda mgombea wa upinzani Lissu. Alikabiliwa na shutuma kali kutoka mataifa ya Magharibi na vyama vya upinzani kwa kudumaza demokrasia, jambo ambalo amelikanusha.

Marehemu Seif Sharif Hamad
Marehemu Seif Sharif Hamad

Wasi wasi unazidi kuongezeka kuwa Tanzania imekumbwa na janga hili hasa baada ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Shariff Hamad, kufariki kwa Covid-19 mwezi Februari, chama chake cha ACT-Wazalendo kilisema.

XS
SM
MD
LG