Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 01, 2022 Local time: 00:26

Watanzania waomboleza kifo cha Rais Magufuli


Hayati John Magufuli

Leo Giza nene limetanda nchini Tanzania na wananchi wa taifa hilo wana simanzi kubwa sana kwa kifo cha Rais John Pombe Magufuli.

Rais Magufuli ndiyo kwanza ameanza uongozi wake wa awamu ya pili baada ya kushinda uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka jana. Mwenzangu Khadija Riyami anaripoti kumuelezea Magufuli.

Rais Magufuli alikuwa na umri wa miaka 61, akijulikana kwa ukali wake katika utendaji kazi ambao ulimfaya akapewa jina la ‘Bulldozer’ lakini mtetezi mkubwa wa wanyonge kutokana na sera za kupigania haki ya taifa la Tanzania kusimamia rasilimali zake ili zifaidishe wananchi na kupambana vikali na rushwa.

Magufuli katika enzi ya uhai wake amekuwa akijivunia mafanikio makubwa aliyoleta katika awamu yake ya kwanza uongozi na kusimamia ujenzi wa miundo na kuelezea kuwa alifanikisha kuiingiza nchi katika uchumi wa daraja la kati.

Marehemu Magufuli ambaye alizaliwa Chato magharibi mwa Tanzania mwaka 1959 alipata shahada ya kwanza kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaa, na kurejea chuoni hapo kama mwalimu na hatimaye kuendelea na masomo hadi kupata shahada ya uzamivu au PhD.

Alianza siasa mwaka 1995 kwa kuchaguliwa kama mbunge katika chama tawala cha CCM na tangu wakati huo Magufuli amekuwa katika baraza la mawaziri kuanzia utawala wa marehemu Rais Benjamin Mkapa hadi Rais Jakaya Kikwete.

Rais Magufuli atakumbukwa kwa kuwa na msimamo mkali sana kuhusu janga la Covid 19 ambalo limeutikisa ulimwengu kwa kusema Tanzania imefanikiwa kutokomeza virusi vya corona kwa sala na kutumia dawa za miti shamba na hivyo kuwataka wananchi wasiwe na khofu kamwe Covid haitaliyumbisha taifa. Na kusema kulikuwa hakuna haja ya kuweka masharti ya kujikinga na virusi hivyo kama ilivyokuwa inafanyika katika nchi nyingine kwingineko barani Afrika na duniani kwa jumla.

Tanzania mara ya mwisho kutoa takwimu kuhusu hesabu ya maambukizi na vifo ilikuwa Aprili 29, 2020. Wakati huo kulikuwa na kesi 509 zilizoripotiwa na vifo 21, kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).

Magufuli kwa wengi anaelezewa kuwa ni mchapa kazi na mkali na mwenye kuweza kuchukua hatua wakati wowote na tangu aingie madarakani amechukua hatua kama vile kuwafukuza kazi watumishi wa umma wakati wowote alipohisi hawatimizi wajibu wao, akiwa na msemo wa ‘kutumbua majipu’ na ‘hapa kazi tu’.

“Nachukia wezi, kwa kweli watakoma. Mwizi anatoka Ulaya au anatoka West, East, South mwizi ni mwizi tu, lazima waule wa chuya, kwa hiyo tutaendelea kubana mianya yote”alisema rais Magufuli.


Moja ya maswala anayosifiwa Magufuli ni jinsi alivyopigania haki ya uchimbaji madini na makampuni ya nje ya Acacia na kampuni mama Barrick hadi pande hizo mbili zikakubaliana Oktoba 2019 kulipa dola milioni 300 na kuipatia serikali ya Tanzania asilimia 16 katika kampuni yao iliyopewa jina la Twiga.

Katika kile kilichoonekana na makundi ya haki za binadamu kama serikali ya Magufuli kuzuia uhuru wa habari utawala huo umefungia magazeti kadha. Amnesty International inasema magazeti ya lugha ya Kiswahili Raia Mwema, Mawio na Mwanahalisi yote yalifungiwa kwa muda baada ya kuchapisha nakala tofauti za kumkosoa rais.

Rais Magufuli katika miezi ya karibuni amekuwa mstari mbele kuelezea alivyoleta mafanikio makubwa katika taifa la Tanzania kwa kuifanya nchi hiyo kuwa ya nchi ya viwanda huku akijivunia nchi hiyo kuingia uchumi wa kati mwaka jana kwa mujibu wa benki ya Dunia.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG