Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Septemba 10, 2024 Local time: 11:25

Viongozi wa dunia watuma rambirambi kufuatia kifo cha Magufuli


Hayati John Pombe Magufuli
Hayati John Pombe Magufuli

Viongozi mbali mbali wametuma salaam zao za rambi rambi kuhusu kifo cha Rais Magufuli, wakielezea kuwa si taifa la Tanzania peke yake ambalo limempoteza kiongozi wake bali bara zima la Afrika na dunia kwa jumla.

Serikali ya Marekani katika salaam zake za rambi rambi kwa watanzania juu ya kifo cha Rais John Magufuli imeahidi kuwa itaendelea kufanya kazi na serikali ya Tanzania kuboresha uhusiano kati ya watu wa Marekani na wa Tanzania.

Katika taarifa yake ya maandishi kupitia msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Ned price, amesema kuwa bado Marekani ina nia ya dhati ya kuendelea kuwaunga mkono watanzania wakati wakitetea heshima ya haki za binadamu na misingi ya uhuru na kufanya kazi katika kupambana na janga la Covid 19. “Tuna matumaini kwamba Tanzania itaweza kusonga mbele katika njia ya kidemokrasia,” taarifa hiyo imeongeza.

Naye Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa hivi leo ametuma salaam za rambi rambi kwa makamu rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaye alitangaza kifo cha Rais Magufuli jana usiku.

Rais Cyril Ramaphosa
Rais Cyril Ramaphosa

Magufuli kiongozi ambaye alijulikana sana barani Afrika na dniani kwa jumla kwa msimamo wake kuhusu janga la Covid 19, amefariki kwa ugonjwa wa moyo.

“Leo tunaomboleza kifo cha mfalme wetu, pia tumepokea kwa masikitiko makubwa sana habari za kifo chake. Nimezungumza na Makamu Rais Samia Suluhu leo asubuhi na kuwasilisha salaam za rambi rambi kutoka kwa wananchi wa Afrika Kusini. Kama mnavyofahamu Tanzania ilisimama kidete katika mapambano ya kugombea uhuru wa Afrika Kusini, walisimamisha juhudi zao za maendeleo kwa ajili yetu sisi,” taarifa ya Ramaphosa imesema.

Nchi Jirani ya Uganda ambapo Hayati Rais Magufuli alikuwa na uhusiano mzuri na Rais Yoweri Museveni, imeelezea kusiskitishwa sana kifo cha Magufuli baada ya wiki kadhaa za wasi wasi kuhusu afya yake. Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Rais Museveni imesema kuwa Magufuli alikuwa kiongozi aliyefanya mambo yake kwa vitendo na ambaye alijikita katika kuwawezesha waafrika mashariki kiuchumi. Tunaungana na watanzania katika kuomboleza kifo cha mtoto wa Afrika. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.”

Rais Yoweri Museveni
Rais Yoweri Museveni

Viongozi mbali mbali kote barani humo wameendelea kutuma salaam za rambi rambi kwa kifo cha Magufuli. Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat amesema, , ‘familia ya Umoja wa Afrika imeungana katika msiba huu mzito na serikali na watu wa Tanzania kwa kifo cha Magufuli. Afrika imepoteza bingwa wa ushirikiano wa kieneo katika eneo la Afrika Mashariki na kiongozi mpenda mageuzi.’ Kwa mujibu w mtandao wa Africa dot cgtn.

Huko Ulaya waziri mkuu wa Uingereza, Boris Johnson ametweet hivi leo akisema ‘nina masikitiko makubwa kusikia habari za kifo cha Magufuli. Sala na maombi yangu yako kwa wapendwa wake na watu wa Tanzania.”

Lazarus Chakwera rais wa Malawi pia ametangaza kuwa nchi yake itaungana na Tanzania katika kuomboleza kifo cha Magufuli kwa siku 14, “ Rais Magufuli alikwa mnara wa kuibuka kwa uchumi barani Afrika na kifo chake ni hasara kubwa kwa bara hili. Malawi inaungana na watanzania kuombolea katika siku 14 zijazo, tunawaombea watanzania wawe na nguvu na ujasiri na kuisaidia serikali yao isonge mbele katika kuendeleza uthabiti na amani katika taifa hilo.’

Viongozi mbali mbali wa Afrika wametweet kuelezea masikitiko yao kwa kifo cha Magufuli. Rais hage Geingob wa Namibia, Paul Kagame wa Rwanda, na Dr. Mokgweetsi masisi wa Botswana.

Salaam za rambi rambi zinaendelea kumiminika nchini Tanzania.

XS
SM
MD
LG