Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 27, 2024 Local time: 04:25

Wapalestina, Waisraeli na dunia washeherekea kusitishwa mapigano


Waumini wa Kiislam wa Palestina wakusanyika kufanya ibada katika uwanja wa msikiti wa al-Aqsa, eneo la tatu kwa utukufu katika dini ya Kiislam, Mei 21,2021.(Photo by AHMAD GHARABLI / AFP)
Waumini wa Kiislam wa Palestina wakusanyika kufanya ibada katika uwanja wa msikiti wa al-Aqsa, eneo la tatu kwa utukufu katika dini ya Kiislam, Mei 21,2021.(Photo by AHMAD GHARABLI / AFP)

Wapalestina, Waisraeli na dunia kwa ujumla wanasheherekea makubaliano ya kusitisha mapigano ya siku 11 kati ya Hamas na jeshi la Israeli.

Viongozi wa dunia wamepongeza juhudi za Misri kuweza kufikia makubaliano hayo baada ya uharibifu mkubwa kwenye ukanda wa Gaza na vifo vya zaidi ya Wapalestina 200 na Waisraeli 12.

Marekani, Umoja wa Mataifa na baadhi ya nchi za Kiarabu zimeahidi kujenga upya Gaza na kutoa wito wa kuanza majadiliano ya dhati ya kupatikana amani ya kudumu huko Mashariki ya Kati.

Kumekuwepo na sherehe usiku kucha kwenye Ukanda wa Gaza baada ya makubaliano kutangazwa na mashambulizi kumalizika huku wananchi wa ukanda huo wakichukulia kuwa ni ushindi mkubwa.

Mkazi wa Gaza anasema leo ni siku ya ushindi ni siku ya uhuru. Ameongeza kusema : "Leo ndiyo siku nzuri kabisa na leo ni siku ya ushindi na siku ya ukombozi, na tunapongeza wanaharakati na upinzani wetu. Na hata kama wanaangamiza Gaza kamili lakini hawawezi kuangamiza imani yetu ya kuwapinga."

Waisraeli wamefurahia pia usitishaji mapigano lakini wengi hawadhani suluhisho la kudumu litaweza kupatikana haraka, kama anavyosema Merav Mkazi wa mji huo.

Merav mkazi wa Jerusalem : "Ninamatumaini tutakuwa na siku zijazo zitakazokuwa nzuri. Ninamatumaini usitishaji mapigano utaheshimiwa na mambo yatakuwa mazuri na tutamaliza mgogoro huu.

Antonio Guterres
Antonio Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewataka viongozi wa Israeli na Palestina kuchukuwa majukumu yao kwa dhati na kuhakikisha wanatanzua matatizo ya msingi yaliyo sababisha mapigano hayo kwa kuanza mazungumzo. Na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuwasaidia Wapalestina na kuleta amani ya kudumu.

Guterres ameeleza kuwa : "Ninatoa wito kwa jumuiya ya Kimataifa kufanyakazi na Umoja wa mataifa kubuni mpango kabambe na kwa haraka kusaidia ukarabati endelevu utakaowasaidia wananchi wa palestina na kuimarisha taasisi zao. "

Rais Joe Biden wa Marekani akipongeza kusitishwa mapigano kati ya Israeli na Hamas amesema hii ni nafasi chanya na ya kweli katika kufikia lengo la kupatikana amani ya kudumu huko Mashariki ya Kati.

Biden Aliongeza : "Marekani inadhamana ya kufanya kazi na Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa kimataifa ili kukusanya msaada wa kimataifa kuwasaidia wananchi wa Gaza katika juhudi za kuikarabati Gaza.

Rais Joe Biden
Rais Joe Biden

Makubaliano ya kusitisha mapigano yamefikiwa kutokana na upatanishi wa Misri na kishinikizo la jumuiya ya kimataifa kufuatia mashambulio ya roketi 4,300 kutoka Gaza yaliyofyatuliwa na kundi la Hamas na makundi mengine ya wanaharakati wa Kiislamu na makombora na mizinga yaliyodondoshwa na jeshi la Israeli kwenye Ukanda wa Gaza.

Wapalestina 232 waliuliwa na Waisraeli 12 pamoja na Wapalestina 1900 waliojeruhiwa. Karibu watu 120,000 wa Gaza wamepoteza makazi yao au kulazimika kuhama.

Maafisa wa Kidiplomasia wanasema Misri inapeleka ujumbe Tel Aviv na maeneo ya Wapalestina ili kufuatilia utekelezaji wa makubliano ya kusitisha mapigano. Rushia, China na nchi za Ulaya zimepongeza mafanikio hayo na kutoa wito wa kuanzishwa mazungumzo ya dhati ya amani ya Mashariki ya Kati.

Mapigano hayo yameongeza sana mivutano kati ya Wayahudi na Waarabu wa Israel na kusababisha ghasia katika miji ya Israeli na kusababisha pia Wapalestina kupambana na walowezi wa Kiyahudi kwenye maeneo yanayokaliwa ya ukanda wa Magharibi na Jerusalem ya Mashariki.

XS
SM
MD
LG