Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Juni 22, 2024 Local time: 09:44

Wasiwasi upo wa kuzuka vita kamili kati ya Israeli na Palestina


Benny Gantz
Benny Gantz

Mashambulizi ya roketi na makombora kati ya Waisraeli na Wapelstina pamoja na ghasia katika miji yenye mchanganyiko wa Waarabu na Wayahudi huko Israeli yamezusha wasiwasi mkubwa kote duniani kuwa pande hizo mbili ziko kwenye ukingo wa vita kamili.

Waziri wa Ulinzi wa Israel Benny Gantz ameapa kutakuwepo na mashambulio zaidi dhidi ya kundi la Hamas na makundi mengine huko Gaza ili kuleta utulivu kamili wa muda mrefu kabla ya kufikiria suala la usitishaji mapigano.
Mataifa duniani yanatoa wito wa kusitishwa maramoja mashambulio hayo huku yakilaani mashambulio yanayowalenga raia.

Wanamgambo wa Kiislamu wamefyetua zaidi ya roketi elfu moja kutoka Gaza kulingana na jeshi la Israel ambalo nalo limefanya mamia ya mashambulio ya anga dhidi ya wapiganaji Wakiislamu katika kanda hiyo na kuharibu kabisa jengo la ghorofa 12 alfajiri ya Jumatano.

Maafa makubwa yameipata família moja huko Gaza ambapo watu watano wafamilia hiyo waliuwawa kutokana na kombora la Israeli.

Shambulizi la Israel katika mji wa Gaza, Jumatano, Mei 12, 2021. Shambulizi hili linafuatia roketi zilizorushwa kutoka Gaza kuelekea Israeli.
Shambulizi la Israel katika mji wa Gaza, Jumatano, Mei 12, 2021. Shambulizi hili linafuatia roketi zilizorushwa kutoka Gaza kuelekea Israeli.

Wakazi wa Gaza wameonekana Jumatano wakiangalia uharibifu uliofanyika jana usiku na Bahaa Khader mkazi wa jengo la Sousi Tower lililoharibiwa na makombora anasema watu walionywa kuondoka kwa haraka kabla ya shambulio kutokea.

Khader, mkazi wa jengo la Sousi Tower, anasema : "Huu ni wendazimu na inaonekana adui amepoteza akili zake kwa kile alichokifanya hapa. Kushambulia jengo hili ni ugaidi dhidi ya watu wa jengo na ni ujumbe mambo yatakuwa magumu zaidi, ujumbe ni wazi."

Mapigano hayo makali kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 7 ilyiopita yamesababisha vifo vya wapalestina 48 wakiwemo watoto 14 huko Gaza na watatu kwenye Ukingo wa Magharibi na Waisraeli watano tangu kuanza siku ya jumatatu.

Msemaji wa polisi wa Israel Mickey Rosenfeld anasema wanaimarisha usalama katika miji yote.

Rosenfeld anaeleza : "Polisi ya Israeli inaendelea kuimarisha usalama kote nchini. Tumeshuhudia mnamo saa 48 zilizopita zaidi ya roketi 900 yaliyofyatuliwa ndani ya Israeli katika maeneo ya watu wanaishi na ni 300 zilizoweza kutua miji mingine imenaswa na mfumo wa ulinzi dhidi ya makombora, Iron Dome.

Mashambulio haya yamechochewa na ghasia zilizokuwa zinafanyaika kwenye uwanja wa msikiti mtakatifu wa Al Aqsa mjini Jerusalem kati ya waumini na polisi na zilifikia kilele chake Ijumaa ya mwisho ya mwezi wa Ramadhani pale Polisi wa Israel walipoingia ndani ya mskiti na kuwashambulia waumini.

Ghasia hizo zimeenea hivi sasa katika miji ya Israeli yenye mchanganyiko wa wakazi wa Kiarabu na Kiyahudi, ambako kumekuwepo na wizi wa ngawira na magari kutiwa moto.

Hali hiyo yote inazidi kuzusha wasiwasi katika pembe zote za dunia. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres amesema ni lazima ghasia zisitishwe mara moja.

Antonio Guterres
Antonio Guterres

Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya uhalifu wa kimataifa Fatou Bensouda kwenye ujumbe wa Twitter anasema huwenda uhalifu umefanyika kutokana na kuongezeka ghasia huko Jerusalem, Gaza na Ukingo wa magharibi.

Kutokana na picha za kusikitisha ambapo wote raia wa Palestina na Waisrael wakionekana wanakimbia ili kuokoa maisha yao, wachambuzi wanasema ni dalili ya ukosefu wa uongozi katika kanda hiyo na Brian Katulis wa taasisi ya Center for American Progress ameiambia Sauti ya Amerika kwamba diplomasia inahitajika kuchukua jukumu kubwa hapa.

Katulis anaeleza : "Hii ni hali tete kabisa. Inaonyesha kwamba kuna ukosefu wa uongozi katika kanda ambapo pande zenye itikadi kali zinatumia kujinufaisha. Wakati wowote pale ghasia zinatumika na makombora kufyatuliwa kiholela tunavoshuhudia kati ya Waisrael na Wapalestina inadhihirisha kwamba mambo hayawezi kudhibitiwa tena na hapa ninadhani Marekani ina nafasi ya kutumia diplomasia kupunguza mivutano.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana tena Jumatano kwa kikao cha dharura juu ya hali huko Mashariki ya Kati. Mwenyekiti wa Umoja wa Africa Moussa Faki Mahamat amelaani vikali mashambulizi ya Gaza na shambulio dhidi ya msikiti wa Al Aqsa, akisema katika taarifa yake kwamba Umoja wa Afrika unaendelea kuunga mkono haki ya Wapalestina kupigania uhuru wa taifa lao la Jerusalem Mashariki kuwa mji wao mkuu.

XS
SM
MD
LG