Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 09, 2022 Local time: 06:13

Trump na mshauri wa usalama wakinzana kuhusu tishio la Korea Kaskazini


Rais Donald Trump, Kulia, Waziri wa Mambo ya Nje Mike Pompeo (kati) na mshauri wa usalama wa taifa White House John Bolton

Rais wa Marekani Donald Trump na mshauri wake wa usalama wa taifa wameonekana kukinzana juu ya uzito wa tishio la Korea Kaskazini lilioko hivi sasa.

Katika ujumbe wa tweet aliotuma Ijumaa kutoka Tokyo, Trump amemjibu John Bolton ambaye siku moja iliyopita aliwaambia waandishi wa habari kuwa “hakuna shaka” kitendo cha Korea Kaskazini kujaribu kombora la balistika la masafa mafupi limevunja azimio la Umoja wa Mataifa.

Kauli ya Bolton ni ya kwanza kutolewa na afisa wa Marekani akieleza kuwa kitendo cha Korea Kaskazini kurusha kombora ni kukiuka azimio la Umoja wa Mataifa.

“Korea Kaskazini ilifyatua baadhi ya silaha hizo ndogo ambazo zimewakera baadhi ya watu wangu na wengine, lakini sio mimi mwenyewe,” Trump amesema katika ujumbe wake wa tweet.

Lakini baadhi ya wachambuzi wanaeleza kuwa kurushwa kwa makombora hayo ni suala lenye kuleta wasiwasi.

“Ni dhahiri kuwa kurushwa kwa kombora kunakiuka vikwazo vilivyowekwa na UN, haijalishi ni la umbali gani. Ukweli ni kuwa majeshi ya Marekani na raia nchini Korea Kusini na Japan tayari wako katika umbali ambao makombora ya Korea Kaskazini yanaweza kuwafikia, na hivyo basi kukubali makombora ya masafa mafupi au ya kati kunaiweka Marekani hatarini, na hivyo hivyo washirika wetu Japan na Korea Kusini,” Kevin Maher, mshauri wa mambo ya usalama Washington na mkuu mstaafu wa Kitengo cha Masuala ya Japan katika Wizara ya Mambo ya Nje, ameiambia VOA.

“Ukweli ni kuwa liko tatizo hata iwapo lengo ni kuonyesha mahusiano binafsi na dikteta Kim Jong Un kuwa yataizuia Korea Kaskazini kuendeleza programu yake ya nyuklia na makombora.”

Rais wa Marekani pia ameeleza ana imani kuwa kiongozi wa Korea Kaskazini “ ataweka ahadi yake kwangu” kwa kuanza kuondoa silaha za nyuklia.

Katika ujumbe wake wa tweet, Trump amesema pia alitabasamu wakati Kim alipomwita Makamu wa Rais mstaafu Joe Biden “ni mtu mwenye ufahamu mdogo.”

Ujumbe wa awali wa tweet wa rais ulikosea jina la mgombea kiti cha urais kwa tiketi ya Demokrat lililosomeka “Bidan” na baadae likarekebishwa.

Na siyo Kim aliyetoa maneno ya kashfa kuhusu Biden, bali ni maoni yaliyokuwa hayana jina yaliyochapishwa na shirika la habari kuu la Korea Kaskazini, ambayo yalimuelezea mwanasiasa wa Marekani kuwa ni “mpumbavu mwenye ufahamu mdogo” na mtu mpuuzi mwenye viwango vya chini kama binadamu.”

Trump amehitimisha ujumbe wake wa tweet kuwa Kim anajaribu “kunitumia ishara” ikimaanisha kuwa kiongozi wa Pyongyang anapendelea kufanya mazungumzo na rais wa hivi sasa wa Marekani na siyo mgombea wa chama cha upinzani.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG