Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 27, 2024 Local time: 04:47

Somaliland yasema haihusiki kabisa na mvutano wa Kenya na Somalia


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akita na mgeni wake Rais wa Somaliland Musa Bihi Abdi.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akita na mgeni wake Rais wa Somaliland Musa Bihi Abdi.

Rais wa Somaliland Musa Bihi Abdi, amesema serikali yake imefurahishwa na juhudi za kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati yake na Kenya na kwamba haihusiki kwa vyovyote vile katika mvutano wa kidiplomasia kati ya Kenya na Somalia.

Matamshi yake Rais huyo yanajiri wakati uhusiano kati ya Kenya na Somalia umekuwa mbaya kiasi cha Somalia kuwafukuza wanadiplomasia wa Kenya mjini Mogadishu baada ya ziara ya Rais wa Somaliland mjini Nairobi.

Katika mahojiano na Sauti ya Amerika, Rais wa Somaliland amesema ziara yake nchini Kenya haina uhusiano wowote na mzozo unaoendelea kati ya Kenya na Somalia na kwamba malengo ya Somaliland ni kuboresha ukuaji wa uchumi na diplomasia kwa manufaa ya watu wake.

Abdi ameishutumu Somalia akisema kwamba imekuwa ikizuia ushirikiano wa Somaliland na nchi zingine kwa muda mrefu.

Rais Abdi anasema : "Tunachofanya ni kuboresha uhusiano kati ya Somaliland na Kenya. Uhusiano kati ya Kenya na Somalia hautuhusu chochote. Iwapo Somalia inaamua kusitisha uhusiano wa kidiplomasia na nchi yoyote inayoshirikiana na Somaliland, jinsi ambavyo wamekuwa wakifanya kwa muda wa miaka 30 iliyopita, tutaona nchi ambayo Somalia itashirikiana nayo.

Rais Uhuru Kenyatta akimkaribisha Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmajo, Ikulu Nairobi 2019.
Rais Uhuru Kenyatta akimkaribisha Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmajo, Ikulu Nairobi 2019.

Somalia imeamurisha wanadiplomasia wote wa Kenya kuondoka Mogadishu ndani ya siku saba kuanzia jana jumanne, huku wanadiplomasia wake mjini Nairobi wakitakiwa kuondoka mara moja.

Viongozi wa Somalia wanadai kwamba Kenya imekuwa ikiingilia maswala yake ya ndani na siasa zake.

Somalia ilichukua hatua hiyo wakati rais wa Somaliland alikuwa nchini Kenya kwa mkutano na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Kulingana na taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari baada ya mkutano huo, viongozi hao walikubaliana kushirikiana katika maswala mbali mbali ikiwemo Kenya kufungua ubalozi mdogo mjini Hargeisa nchini Somaliland ifikapo Machi mwaka 2021, kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya Nairobi na Hargeisa, kuimarisha sekta za biashara, kilimo, teknolojia, elimu, usalama, na ushirikiano kati ya maafisa wenye ujuzi wa juu kati ya serikali hizo mbili, miongoni mwa mambo mengine.

Wachambuzi wa siasa za Pembe ya Afrika wanasema kwamba Somalia haitaki nchi yoyote kushirikiana na Somaliland moja kwa moja.

Msemaji wa Serikali ya Kenya Cyrus Oguna amesema Kenya itatumia njia za kidiplomasia kusuluhisha mzozo kati yake na Somalia.

Somaliland ilijiondoa kutoka Somalia mnamo mwaka 1991 japo uhuru wake haujatambuliwa na umoja wa mataifa, Umoja wa Afrika, AU.

Kenya inakuwa nchi ya pili kuingia katika mgogoro na Somalia baada ya Guinea kuhusiana nah atua ya kushirkiana na Somaliland.

XS
SM
MD
LG