Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Aprili 16, 2024 Local time: 07:11

Somalia yasitisha utoaji wa viza kwenye uwanja wa ndege kwa wageni kutoka Kenya


Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed maarufu kama Farmajo.
Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed maarufu kama Farmajo.

Serikali ya Somalia Jumatatu ilisimamisha utoaji wa vibali vinavyotolewa kwenye uwanja wa ndege nchini humo kwa wageni kutoka Kenya.

Badala yake iliwashauri wote wanaosafiri nchini humo kuomba Viza kwenye ubalozi wake mjini Nairobi kabla ya kusafiri.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation la Kenya, amri hiyo itaanza kutekelezwa Decemba 13.

Ofisi ya uhamiaji ya Somalia imesema kuwa hatua hiyo imepelekewa na tahadhari dhidi ya maambukizi ya Covid19.

Taarifa zinaongeza kusema kuwa watu wenye vyeti vya kusafiria vya kidiplomasia watahitajika kupata idhini kutoka kwa wizara ya mambo ya kigeni mjini Mogadishu kabla ya kusafiri nchini humo.

Mwezi Novemba mwaka huu, Somalia ilifungua tena ubalozi wake mjini Nairobi baada ya kufungwa kwa miaka 10 kufuatia ushindi wa kesi dhidi ya mwekezaji binafsi aliekuwa ameununua kwa njia ya magendo wakati mapigano yakiendelea Somalia.

Jengo la ubalozi, lililo eneo la Westlands mjini Nairobi, lilinunuliwa mwaka wa 1972 na limekuwa likikarabatiwa kwa miaka miwili iliopita.

Sasa ubalozi huo unatarajiwa kufunguliwa tena ukisimamiwa na balozi wa Somalia nchini Kenya, Mohamoud Ahmed Nur Tarsan.

-Imetayarishwa na mwandishi wa VOA Harrison Kamau, Washington DC

XS
SM
MD
LG