Tangazo hilo limetolewa wakati msimu wa ibada ya Hija ukiwa umekaribia, na mahujaji kutoka pande mbalimbali za dunia wakiwa tayari safarini kuelekea Makka kwa ajili ya kutekeleza ibada hiyo na kuzuru maeneo matakatifu.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia imesema uamuzi huo umefikiwa baada ya Shirika la Afya Duniani, WHO, kutangaza kuwa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini DRC ni suala la dharura inayohitaji kushughulikiwa na jumuia ya kimataifa.
''Kwa hivyo mpango wa kutoa viza kwa watu wanaoingia kutoka DRC umesimamishwa, kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa mahujaji,'' wizara imeeleza.
Pia taarifa ya wizara imeeleza kuwa wakati wa Hija, mahujaji wataweza kufikia huduma za dharura kwa kupiga simu numbari 911, kwa tukio lolote la dharura, iwapo amepotea njia au anahitaji maelekezo, msaada wa barabarani, huduma ya dharura ya kiafya, kukiwa na mnyama njiani au kupotelewa na kitu chochote.
Imetangaza kuwa kuna timu ya vijana wa Saudi Arabia ambao wametayarishwa kutoa msaada huo saa 24 na siku saba za wiki.
Vijana hao wanazungumza lugha mbalimbali zikiwemo Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, Kiindonesia, Kiurdu.
Ujumbe wa maandishi umetumwa kwenye mitandao ya simu ukisema : Wapendwa mahujaji, kuwahudumia ni heshima kubwa na usalama wenu ni jukumu letu. Polisi wako tayari kutoa msaada kwa huduma za dharura mnazohitaji mkipiga simu nambari 911.
Kituo cha Taifa cha Operesheni za Usalama katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia kilizindua huduma ya kituo cha nambari 911 miaka mitano iliyopita mjini Makka na hivi sasa vituo vingine vitatu vimefunguliwa miji mingine ikiwemo Riyadh, Shargiyah na Madinah.
Vituo hivyo vina mawasiliano kwa njia ya Twitter, vikitoa taarifa mpya kuhusiana na vimbunga vya majangwani, kufungwa kwa njia kuu kunapotokea ajali za gari na wanyama wanapoonekana barabarani.