Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Julai 22, 2024 Local time: 18:08

Pompeo : Mfalme, mwana mfalme Saudia wako tayari kuwawajibisha waliomuuwa Khashoggi


Waziri wa Mambo ya Nje Mike Pompeo akiwa na mwana wa mfalme
Waziri wa Mambo ya Nje Mike Pompeo akiwa na mwana wa mfalme

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amesema Mfalme wa Saudi Arabia Salman na mwana mfalme Mohamed Bin Salman wamekiri wale walio husika na mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi ni lazima wawajibishwe.

Pompeo aliyasema hayo Jumatatu baada ya kukutana na viongozi wa Saudi Arabia mjini Riyadh.

Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Marekani amesema wote mfalme na mwana mfalme walisisitiza nia yao ya dhati kuwawajibisha wote ambao walihusika kumuua Kashoggi baada ya kwenda kwenye ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul nchini Uturuki October, 2018.

Awali Saudi Arabia ilisema aliondoka kwa salama kwenye eneo hilo la ubalozi, lakini baadae ilikiri aliuwawa huko katika kile ambacho maafisa wa Saudi Arabia walisema operesheni ya kihuni.

Uturuki imesema amri ya kumuuwa mwandishi huyo wa Gazeti la Washington Post ilitoka ngazi ya juu ya serikali ya Saudi Arabia, lakini maafisa wa ufalme huo walisisitiza mwana mfalme hakutoa amri yoyote.

Mnamo mwezi Disemba, Baraza la Seneti la Marekani liliikemea Saudi Arabia, likimlaumu mwana wa mfalme kuhusika na mauji ya Khashoggi na kutaka kusitishwa kwa misaada ya Marekani kwa ushirika wa majeshi yanayo ongozwa na Saudi yanayo pigana Yemen.

Pompeo na Mohammed bin Salman walikubaliana Jumatatu juu ya umuhimu wa kuendelea na juhudi za kusitisha vita Yemen, hasa katika bandari ya Hodeida.

Ubalozi wa Marekani Saudi Arabia ulituma picha kupitia akaunti yake ya Tweet kuonyesha mkutano baina ya Pompeo na mwana mfalme na amesema, “Suluhisho kamili la kisiasa ni njia pekee ya kumaliza vita hivyo.”

Tangu mwaka 2015, Saudi Arabia imekuwa ikiongoza ushirika wa majeshi yanayo fanya mashambulizi ya anga nchini Yemen na juhudi nyingine za kivita kuisaidia serikali ya Yemen katika mapambano yake dhidi ya waasi wa Kihouthi ambao wanaushikilia mji mkuu na maeneo mengine.

Marekani imekuwa ikitoa msaada kwa majeshi yanayo ongozwa na Saudi Arabia, ikiwemo kuwajazia mafuta na misaada ya maandalizi mengine.

Pompeo anakaribia kumaliza ziara yake huko Mashariki ya Kati ambapo amekuwa akiwahakikishia washirika wa Marekani juu ya utaratibu kufuatwa katika hatua ya majeshi ya Marekani kuondoka Syria na kuomba washirika hao waunge mkono jitihada za Marekani kuifanya Iran ibadilike kile uongozi wa Trump unachokiita ni tabia hatarishi ya Iran.

Kutoka Saudi Arabia Pompeo atakwenda Oman Jumatatu, lakini atafupisha ziara yake iliyobakia ili kuhudhuria maziko ya mwanafamilia. Msemaji wa Pompeo amesema ataelekea Kuwait tarehe itakayo pangwa baadae.

XS
SM
MD
LG