Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Julai 14, 2024 Local time: 07:51

Kenyatta aamuru kuondolewa vikwazo vya kibiashara dhidi ya Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akihutubia Mabunge Mawili ya Kenya (Bunge la Taifa pamoja na Bunge la Senate la Kenya kwa pamoja Jijini Nairobi leo tarehe 05, Mei, 2021. Picha na Ikulu, Tanzania.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameamrisha kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara kati ya Kenya na Tanzania, huku akimwagiza Waziri wa Kilimo nchini humo, Peter Munya kuondoa utata unaohusu uingizaji wa mahindi ya Tanzania katika kipindi cha wiki moja.

Rais Kenyatta alisema hayo Jumatano alpokuwa na mgeni wake Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan walipokuwa wanakutana na jamii ya wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Kenya na Tanzania jijini Nairobi,

Aidha, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anayeendelea na ziara yake huko Kenya, ameeleza kuwa Tanzania iko tayari kufanya biashara na Kenya wakati wote bila vikwazo vyovyote.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akihutubia Mabunge Mawili ya Kenya (Bunge la Taifa pamoja na Bunge la Senate la Kenya kwa pamoja Jijini Nairobi leo tarehe 05, Mei, 2021. Picha na Ikulu, Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akihutubia Mabunge Mawili ya Kenya (Bunge la Taifa pamoja na Bunge la Senate la Kenya kwa pamoja Jijini Nairobi leo tarehe 05, Mei, 2021. Picha na Ikulu, Tanzania.

Kiongozi huyo amesisitiza juu ya nia ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara na uwekezaji kwa kuondoa vizuizi vya kibiashara ili kufungua uwezo wa nchi mbili wanachama wa Jumuiya ya Umoja wa Afrika Mashariki.

Katika mkutano huu, Rais Kenyatta amesema wawekezaji wa Tanzania wanastahili kuingia Kenya na kufanya biashara bila vibali ilimradi watii sheria za Kenya.

Kiongozi huyo wa Kenya amewaonya mawaziri dhidi ya kutumia muda mwingi kukaa ofisini badala ya kushirikiana kuondoa matatizo yanayo wakumba raia wa nchi hizi mbili.

Mgeni wake Rais Samia, ameeleza kuwa Tanzania iko tayari kufanya biashara na Kenya wakati wote ili kuongeza uwezo wa bidhaa zinazoingizwa katika mataifa hayo kuzalisha ajira kwa raia wake.

Rais Samia amekariri katika hotuba yake, kuwa Kenya na Tanzania ni nchi zilizo na uwezo mkubwa, na uwezo huo unaweza kuonekana tu iwapo patakuwapo na ushirikiano wa kiwango cha juu kati ya Kenya na Tanzania.

Mawaziri wa Kilimo na Biashara kutoka pande mbili aidha wamefanya kikao cha faragha na kukubaliana kukutana tena kwa kipindi kisichozidi wiki mbili kutatua vikwazo vinavyoleta mifarakano ya kibiashara na uwekezaji kati ya nchi mbili.

Mashirika ya kibiashara ya kiserikali na ya kibinafsi yamekubaliana kuongeza wigo wa kufanya biashara, nia ya kuondoa vikwazo visivyokuwa vya kodi, kuongeza thamani ya biashara na kuongeza ushirikiano kupitia heshima na uzoefu wa ufanyaji biashara kwa kiwango cha juu kama alivyoeleza Waziri wa Biashara na Uwekezaji, Betty Maina.

XS
SM
MD
LG