Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 15:11

Mahakama Kenya yapinga uteuzi wa mawaziri wasiopitishwa na bunge


Rais Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta

Mahakama Kuu ya Kenya imeamuru kuwa hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kuwateua mawaziri nane katika awamu yake ya pili ya uongozi, bila ya kupitishwa na bunge, ni kinyume cha sheria.

Jaji Antony Mrima ameeleza kuwa nafasi ya Katibu Mratibu wa Wizara ni kinyume cha sheria kwa sababu haipo kwenye katiba ya nchi hiyo. Hata hivyo, serikali imesema kuwa itakata rufaa kupinga uamuzi huo.

Mawaziri

Mawaziri hao wanane walisalia baada ya muhula wa kwanza wa serikali ya Rais Kenyatta, kukamilika, kwa sababu hawakupitishwa na bunge la Kenya.

Baadhi ya mawaziri hao ni Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang’I, waziri wa Kawi Charles Keter, Waziri wa Utalii Najib Balala, Waziri wa Mambo ya Nje Rayechelle Omamo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia Joe Mucheru, Waziri wa Michezo Amina Mohamed, Waziri wa Uchukuzi James Macharia na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa.

Jaji Antony Mrima

Jaji Antony Mrima pia ameeleza kuwa uamuzi wa Rais Kenyatta wa Januari 26, 2018, wa kutangaza kwamba ameunda nafasi mpya ya usimamizi kwenye wizara zote 22, yaani nafasi mpya za makatibu waratibu wa wizara ni kinyume cha sheria kwa sababu hazitambuliki katika sheria za nchi.

Nafasi hizi nyingi ambazo zimesimamiwa na baadhi ya watu ambao hawakufaulu kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2017, hao wakitajwa kuwa na ushawishi wa aina fulani na kuonekana kufanya juhudi za kufanikisha kuchaguliwa kwake katika uchaguzi huo.

Makatibu wa Kudumu

Jaji Mrima, aidha, ameeleza kuwa nyadhifa za makatibu wa kudumu ni lazima zitimize mahitaji ya kijinsia ya theluthi mbili huku akiamuru kuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali Paul Kihara Kariuki anastakiwa kwa kipindi cha siku thelathini kuwasilisha usajili wa maafisa hawa, nyadhifa zao, kuonyesha iwapo wametimiza vipengele vilivyopo katika uteuzi wa maafisa wa serikali.

Mahakama hiyo pia imebatilisha uteuzi wa makatibu wa kudumu ambao hawakutambuliwa au kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Umma kupitia mchakato mzima ulio na vigezo vya uajiri.

Uamuzi huu wa Jaji Mrima unatokana na ombi la mwanaharakati Okiya Omtata, ambaye ameieleza mahakama hiyo kuwa nyadhifa hizi ni haramu na hivyo maafisa husika hawawezi kuendelea kulipwa kutoka kwenye mfuko wa fedha za umma wakati wa kuhudumu katika nyadhifa hizo. Omtata aidha, ameeleza kuwa wakati wa uteuzi huo, Kenya ilikuwa inakumbana na kiwango cha juu cha gharama ya mishahara ya wafanyakazi wa umma.

Serikali Kukata Rufaa

Hata hivyo, msemaji wa chama tawala Jubilee, na vile vile waziri katika serikali ya Rais Kenyatta, Raphael Tuju, ameeleza kuwa serikali itapinga uamuzi huo katika mahakama ya rufaa. Tuju, akizungumza kwenye kituo cha televisheni cha Citizen Jumanne usiku, ameeleza kuwa katiba ya Kenya inampa rais uwezo wa kuunda nafasi muhimu katika serikali yake.

“Tuna uwezekano wa kwenda kwenye korti ya rufaa kama serikali na tunajua pia kwamba kifungu cha katiba ya 2010 cha 132 kinatoa maelekezo kwa rais kwa kushauriana na tume ya utumishi wa umma kuunda nafasi yoyote katika utumishi wa umma au serikalini na iwapo korti haikujua hili au korti ilipuuza tuna mahakama ya rufaa ambapo hoja hiyo itaendelezwa kwa hivyo sioni sababu yoyote ya kuwa na hofu,”ameeleza.

Aidha, Tuju amesema kuwa hakuna hofu kwenye baraza la mawaziri, na kazi inaendeleea kama kawaida licha ya uamuzi wa mahakama kuu.

Uamuzi wa Jaji Mrima hata hivyo, hautatekelezwa kwa sasa kwa kile amekitaja kuwa ni kusambaratisha serikali wakati inapambana na janga la virusi vya Corona.

XS
SM
MD
LG