Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 14, 2024 Local time: 10:10

Kenya yatangaza kanuni mpya kukabiliana na COVID-19


Rais Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta

Kenya imegubikwa na wimbi jipya na la tatu la maambukizi ya virusi vya Corona wakati taifa hilo la Afrika Mashariki likiadhimisha mwaka mmoja baada ya kurekodi kisa cha kwanza cha maambukizi hayo Machi 12, 2020, Rais Uhuru Kenyatta amethibitisha Ijumaa.

Akizungumza kutoka ikulu ya Nairobi, Rais Kenyatta ametangaza kuwa serikali yake inaongeza kipindi cha katazo la raia wake kutoka nje kati ya saa nne usiku na saa kumi alfajiri kwa miezi mingine miwili.

Wanasiasa nchini Kenya wamekuwa wakihudhuria mikutano mikubwa ya kisiasa kila wiki na wanaohudhuria wanaonekana kutofuata maagizo ya kujikinga. Wanaoandaa mikutano hawavai barakoa na mara nyingi wanaonekana kusalimiana na kupiga pambaja. Mikutano hii inatajwa kuwa chanzo cha kuambukizana kwa wingi.

Raila Odinga, kiongozi wa Orange Democratic Movement, Alhamisi, kupita taarifa kwa vyombo vya habari, ametangaza kuambukizwa na virusi vya Corona siku chache baada ya kuhitimisha msururu wa mikutano ya kisiasa katika majimbo ya Pwani ya Kenya. Kiongozi huyo anaendelea kupokea matibabu katika kituo cha The Nairobi Hospital.

Raila Odinga
Raila Odinga

Kenya pia, katika kipindi hiki imeshuhudia vifo vya wanasiasa wengi, wengine wakitajwa kufariki kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona.

Rais Kenyatta amepiga marufuku mikutano yote ya kisiasa nchini humo na kuvitaka vyombo vya usalama kuwakamata wote wanaokaidi maagizo hayo,“ninaelekeza kwamba aina zote za mikusanyiko ya kisiasa imeharamishwa kwa kipindi cha siku 30, kuanzia saa sita usiku mnamo Machi 12, 2021,” Kenyatta ameongeza.

Hafla za mazishi zimeratibiwa kufanyika tu katika kipindi cha saa 72 baada mtu kuthibitishwa kufariki na kwamba ni watu mia moja pekee ndio wanaoruhusiwa kuhudhuria.

Raia wa Kenya wamekuwa na matumaini kuwa serikali ingelegeza masharti ili kuendelea na shughuli zao za kawaida, lakini rais Kenyatta ameeleza kuwa “gharama ya uamuzi huu wa ujasiri kwa uchumi wetu ilikuwa kubwa. Walakini, faida ya hatua ya haraka ya sera haina kipimo kwa maisha ya binadamu yaliyookolewa”

Kwa mujibu wa takwimu za serikali, Kenya imepoteza zaidi ya watu 1,879 katika janga hili na kutokana na onyo la wataalam wa afya, iwapo hapangechukuliwa maamuzi mazito na ya ujasiri “tungekuwa na maambukizi takriban milioni moja kitaifa kufikia Krismasi 2020 na vifo 150,000. Mifano mingine ilitabiri matokeo mabaya zaidi” rais Kenyatta amesisitiza.

Kenyatta amefichua kuwa taifa limepoteza takriban shilingi bilioni 560 za pato la taifa kutokana na mtikisiko wa uchumi uliosababishwa na janga la Corona na kukariri kuwa “hii ndio bei ambayo tulilazimika kulipa mwaka 2020 kwa maamuzi ya ujasiri tuliyoyachukua kudhibiti mkwambo huu kiuchumi.”

Mwandishi wetu wa Nairobi, Kennedy Wandera, anaarifu kuwa serikali ya Kenya imekariri kuwa itaendelea kufanya maamuzi yake kutokana na sera ya kisayansi. Rais Kenyatta, aliyehutubia taifa, akieleza kuwa “ushahidi wa mwanzo wa kisayansi kwa mwaka mmoja uliopita umetuonesha kuwa tunapozidisha vizuizi, viwango vya maambukizi ya jamii vinapungua, maambukizi ya virusi yanapungua kwa ujumla”

Kenya imeanza zoezi la kuwapa chanjo raia wake milioni 1.25 katika awamu ya kwanza inayojumuisha wahudumu wa afya wapatao laki nne na walimu wapatao elfu 15,000 katika majimbo yake 47 kwa kutumia dozi milioni 1.02 ya AstraZeneca katika awamu ambayo pia inajumuisha maafisa wakuu wa serikali walio mstari wa mbele kutekeleza maagizo ya serikali.

Serikali ya Kenya haijaeleza hili wimbi jipya ni la aina gani au linahusishwa na nchi gani, na maafisa wa afya wanaeleza kuwa jiji la Nairobi linaendelea kushuhudia idadi ya juu mno ya wagonjwa wanaolazwa na kuhitaji huduma za dharura katika vyumba vya wagonjwa mahututi.

Waziri mratibu wa afya Mercy Mwangangi mbele ya kamati ya bunge ya afya, ameeleza wabunge, Jumatano, mahitaji ya vyumba vya wagonjwa mahututi yameongezeka na vile vile mahitaji ya vifaa vya kupumulia.

“Tunashuhudia ongezeko kubwa la mahitaji ya vyumba vya wagonjwa mahututi, ICU. Kuanzia jana, ICU zote jijini Nairobi zilikuwa zimejaa, ”alisema Mwangangi.

Waziri Mutahi Kagwe
Waziri Mutahi Kagwe

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe tayari ameonya kuwa iwapo raia wa Kenya watachukulia kimzaha janga la Corona, taifa litashuhudia mahangaiko makubwa mno “nieleze kwamba tunakaribia kuanza kipindi kingine kigumu, lakini pia tunaweza kushinda kipindi hiki baada ya kushinda vipindi hivyo vingine viwili, iwapo tu tutazingatia kabisa masharti yaliowekwa na serikali."

Baada ya kupokea chanjo ya dozi milioni 1.02 ya AstraZeneca, Kenya imetangaza kuwa imepokea msaada wa dozi 100,000 za chanjo ya Oxford-AstraZeneca kutoka India ili kusaidia katika juhudi za kuwachanja raia wake dhidi ya virusi vya Corona.

“Chanjo hii iko katika hali nzuri. Watu wanapaswa kujitokeza wakati zamu yao itakapofika kupata chanjo, "alisema waziri Kagwe.

Lakini wakati maafisa wa ngazi ya juu serikalini wanaeleza kuwa wanasubiri Shirika la Afya Duniani WHO kutoa maelezo zaidi kuhusu usalama na ubora wa chanjo ya Johnson & Johnson, Sputnik, Sinovac, SinoPharm na Novavax na Pfizer, Bodi ya mfuko wa Uwekezaji wa moja kwa moja wa nchi ya Urusi, Russia RDIF, imetangaza kuwa Kenya ni miongoni mwa mataifa 48 ambayo yameidhinishwa kupokea chanjo ya Sputnik kwa matumizi ya raia wake.

Machi 3, Kenya imepokea chanjo ya dozi milioni 1.02 ya AstraZeneca ikiwa ni sehemu ya dozi milioni 3.56 ambazo Kenya imeagiza kupitia mpango wa kimataifa wa mataifa masikini na yaliojiunga na mfumo wa muungano wa chanjo maarufu kama GAVI. Mpango huo unaojulikana kama COVAX unapania kusambaza chanjo kwa mataifa yanayoendelea na yalio na kipato cha chini.

Imetayarishwa na mwandishi wetu wa Nairobi, Kennedy Wandera.

XS
SM
MD
LG