Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 09:00

Jeshi lamuondoa Rais Omar al-Bashir madarakani Sudan


Rais Omar al-Bashir (kulia),
Rais Omar al-Bashir (kulia),

Waziri wa Ulinzi wa Sudan Awad Mohamed Ahmed Auf ametangaza kuwa kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir ameondolewa madarakani na anashikiliwa mahala penye usalama.

Akizungumza kupitia Televisheni ya Taifa ya Sudan waziri huyo amesema kutokana na hali hiyo ametangaza hali ya dharura ya miaka mitatu na amri ya kutotoka nje wakati wa usiku kwa muda wa mwezi mmoja.

Amesema kwamba baraza la mpito linaundwa na litabaki madarakani kwa miaka miwili.

Baraza la mpito

Akilihutubia taifa kupitia televisheni ya taifa Auf alisema baraza la mpito litakuwa na jukumu la kutayarisha uchaguzi utakaofanyika wakati muda wa mpito ukimalizika.

Hata hivyo, wanaharakati waloitisha maandamano ya miezi minne mfululizo dhidi ya Rais Bashir wamepinga taarifa ya waziri wa ulinzi ya kutangaza muda wa mpito.

Wanaharakati hao wa chama cha wafanyakazi ambao ni wanataaluma mbalimbali wameitisha maandamano siku ya Jumamosi na kuwataka waandamanaji warejee tena kukaa nje ya makao makuu ya jeshi hilo wakishinikiza kuundwa kwa serikali ya kiraia.

Awali viongozi wao walisema watakubali tu serikali ya kiraia ambayo itajumuisha viongozi wa upinzani.

Taarifa za kujiuzulu Bashir

Taarifa zaidi zinaeleza Rais al-Bashir amejiuzulu, kufuatia shinikizo la jeshi la nchi hiyo baada ya miezi minne ya maandamano yakipinga utawala wake uliodumu kwa miaka 30.

Chanzo cha habari katika jeshi la Sudan kimeifahamisha VOA kuwa Rais huyo alikuwa kizuizini nyumbani wakati viongozi wa jeshi na viongozi wa siasa Alhamisi asubuhi wakizungumzia utaratibu wa serikali ya mpito.

Kufungwa kwa uwanja wa ndege

Ripoti zinaeleza vyombo vya dola vimefunga uwanja wa ndege mkuu na kuwakamata maafisa na viongozi wa jeshi ambao ni watiifu kwa al-Bashir.

Wakati huohuo Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa vikosi vya Sudan vimefanya upekuzi katika makao makuu ya harakati za Kiislam za Bashir, ambacho kinaendesha chama chake cha National Congress Party.

Hata hivyo msemaji wa chama hakujibu ombi la VOA kutoa maoni yake.

Mahojiano maalum na mmoja wa waandamanaji

Waandamanaji Sudan wapinga serikali ya muda
please wait

No media source currently available

0:00 0:02:55 0:00

Waandamanaji washeherekea

Waandamanaji wamekuwa wakisheherekea nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum.

Wanaharakati waloitisha maandamano ya miezi minne hivi sasa dhidi ya Rais Bashir wamepinga taarifa ya waziri wa ulinzi ya kutangaza muda wa mpito.

Kuondolewa madarakani kwa al-Bashir ni baada ya maandamano yaliyoanza kufuatia ongezeko la bei ya mkate, na baadaye bei ghali ya mafuta, na hapo tena upungufu wa chakula na ukosefu wa pesa za kigeni, waandamanaji wakilijitokeza mitaani na kumtaka aondoke madarakani kwa usimamizi mbovu wa uchumi.

Jinsi mapinduzi yalivyoanza

Wakati maandamano yalipoanza, hapo Disema 19, 2018, Bashir, alisema waandamanaji walikuwa vibaraka wa mataifa ya magharibi na kwamba maandamano yao yalikuwa sawa na vilio vya vyura, akisisitiza kwamba mabadiliko nchini Sudan, yangeweza tu kutekelezwa kwa njia ya kidemokrasia.

Al-Bashir alichukua madaraka mwaka 1989 kutokana na mapinduzi yaliyofanywa na chama cha Kiislamu na mara moja kutangaza hali ya dharura kote nchini katika juhudi za kukandamiza upinzani.

Sikiliza mahojiano maalum juu ya mapinduzi ya Sudan

Mapinduzi Sudan : Bado waandamanaji hawajaridhika, wanataka serikali ya kiraia
please wait

No media source currently available

0:00 0:08:01 0:00

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.


XS
SM
MD
LG