Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 07, 2024 Local time: 11:36

Afrika yatafuta mwenyeji wa eneo huru la biashara kuunganisha masoko yake


Ramani ya Afrika
Ramani ya Afrika

Viongozi wa kiafrika watafanya maamuzi siku ya Jumapili taifa gani litakuwa mwenyeji wa makao makuu ya eneo huru la biashara barani humo, ambalo litalenga hatimaye kuwaunganisha watu bilioni 1.27 barani humo na pato lao la jumla la taifa ambalo ni dola trilioni 3.4.

Viongozi katika mkutano wa Umoja wa Afrika unaofanyika Niger pia watapanga tarehe ya kuanza biashara eneo huru la biashara ambalo litajulikana kama African Continental Free Trade, matafia 52 kati ya 55 wametia saini makubaliano hayo.

Umoja huo hatimaye unataka kuondoa vikwazo vya biashara na ushuru kati ya mataifa wanachama.

Kwa mujibu wa kanuni za AU, wanachama wake wote wanaweza kuwasilisha maombi ili kuteuliwa kuwa makao makuu ya eneo huru la biashara. Kenya, Ghana, Eswatini, Madagascar na Misri wamewasilisha maombi. Ethiopia na Senegal waliamua kujitoa katika ushindani huo.

Walio katika ushindani wa sasa wamegawanyika katika kanda kuu za bara hilo: Kenya inatokea mashariki, Ghana kutoka magharibi, eSwatini kutoka kusini wa Afrika, Madagascar inawakilisha visiwa vya bahari ya Hindi na Misri inawakilisha eneo la kaskazini.

Misri ambayo pia inashikilia urais wa AU mwaka huu imekuwa ikihamasisha na kujitaja kuwa kiini katika biashara barani Afrika.

Misri ni moja ya wanachama wa siku nyingi wa Umoja wa Afrika na inafurahia uhusiano wenye nguvu na mataifa mengine ya Afrika, amesema afisa wa kutoka wizara ya biashara Misri na kuongeza kuwa wana vigezo vyote vinavyohitajika.

Kenya na Misri tayari ni wenyeji wa ofisi za taasisi za kimataifa na pia wana mashirika ya ndege yanayotajika sana barani humo.

Kenya ni mwenyeji wa makao makuu ya idara za Umoja wa Mataifa kwa mazingira na maendeleo mijini. UNEP na UN- Habitat. Misri ni mwenyeji wa makamo ya Africa Export Import Bank.

“Nairobi ni eneo la kiasili sana kwa taasisi kama hiyo. Ni rahisi kufika sehemu yoyote katika bara hilo kutoka hapa Nairobi,” Peter Munya, waziri wa biashara wa Kenya amewaambia waandishi wa habari.

Taifa dogo la eSwatini ambalo zamani lilikuwa linajulikana kama Swaziland, limepata uungaji mkono kutoka taasisi ya kieneo ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADCC).

Taifa lolote ambalo litachaguliwa kuwa mwenyeji wa makao makuu ya biashara litapata fursa ya kufungua milango ya ajira kwa raia wake na kupata msaada wa fedha kwa ajili ya sekta za usafiri na utalii.

AU inataka kuongeza biashara yake mpaka asilimia 25 – 36 kwa mwaka ndani ya bara hilo katika muda wa kipindi cha miaka mitano, kutoka asilimia 18 kiwango cha sasa, na kuvutia uwekezaji wa muda mrefu kutoka makampuni makubwa ya utengenezaji magari duniani.

Siku ya Jumapili viongozi wa AU mbali ya kuteua nchi ambayo itakuwa mwenyeji wa makao makuu ya biashra huru, pia watazindua kanuni zinazohusu masuala kama vile biashara huru, kuondolewa kwa vikwazo vya ushuru na mifumo ya malipo .

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Khadija Riyami, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG