Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Novemba 30, 2022 Local time: 23:16

AU yakubaliana kuimarisha taasisi zake kuboresha umoja, usalama na hali za wakimbizi


Kikao kilichomalizika cha Umoja wa Afrika nchini Ethiopia, Februari 11, 2019.

Mkutano wa kila mwaka wa viongozi na wakuu wa serikali wa nchi za Afrika umemalizika mjini Addis Ababa Jumatatu baada ya kujadili masuala ya mabadiliko ya taasisi za umoja huo, usalama na suala la wakimbizi.

Wakati wa mkutano huo wa siku mbili, rais Paul Kagame wa Rwanda alimkabidhi uwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) rais Abdel Fatah el Sissi wa Misri aliyepokea zamu ya uongozi kwa mwaka mmoja .

Mkutano wa 32 wa viongozi wa umoja wa Afrika ulianza jana Jumapili katika mji mkuu wa Addis Ababa kwa kujadili masuala muhimu ya wakati huu barani humo ikiwa ni pamoja na suala la watu kulazimika kukimbia makazi yao, amani na usalama.

Viongozi kutoka mataifa 54 walikutana chini ya mada kuu ya mwaka huu ya Wakimbizi, wanaorudi nyumbani na walokoseshwa makazi, IDPs, katika lengo la kutafuta suluhisho la kudumu juu ya suala la kulazimika kuhama makazi barani afrika.

Juhudi za mageuzi katika utawala wa taasisi za AU na kuipatia kamisheni ya umoja huo nguvu zaidi ni kati ya mambo yaliyopendekezwa na Rais Paul Kagame alipokuwa mwenyekiti wa umoja huo. Wachambuzi wanasema mambo hayo yanajadiliwa ingawa kuna mvutano kati ya wanachama juu ya namna ya kutekeleza mageuzi hayo.

Rais Sisi kwa upande wake anaonekana atazingatia zaidi masuala juu ya usalama, kulinda amani na kazi za kukarabati baada ya vita, kutokana na hotuba yake ya ufunguzi.

Abdelfatah el sisi amesema Ingawa tunafanya kila tuwezalo kupunguza migogoro na vita katika bara letu na mpango wetu wenye matarajio makubwa ya kunyamazisha bunduki kote katika bara hili ifikapo 2020, nyote mnafahamu njia ingali ndefu mbele yetu kuzima vita barani Afrika.

Kwa upande wake Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres akizungumza kwenye mkutano huo ameeleza matumaini yanaonekana barani humo.

Amesema uchaguzi wa amani huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mali na Madagascar, mikataba ya amani iliyofikiwa Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati na kumalizika kwa uhasama kati ya Ethiopia na Eritrea ni ishara ya wimbi la matumaini linalonguruma barani humo.

Antonio Guterres aisifia Afrika

Licha ya changamoto zake wenyewe za kijamii, kiuchumi na kiusalama serikali za Afrika na watu wake wameacha mipaka na mioyo yao wazi kwa ajili ya mamilioni ya wenye haja ya kupata hifadhi.

Viongozi wa AU wanazungumzia pia suala la kuanzishwa mfumo wa biashara huru katika bara zima.

Lakini wachambuzi wanasema hiyo ingali ni changamoto kubwa kwamba tangu mataifa 44 kukubaliana juu ya mkataba wa kuanzishwa biashara huru barani humo, CFTA, ni mataifa 19 tu yaliyokwisha idhinisha mkataba huo wakati inahitaji mataifa 22 kuweza kuutekeleza.

Kabla ya mkutano kuanza wakati wa kuzindua sanamu ya Haile Selassie ndani ya ukumbi wa jengo kuu la AU kulizuka msongamano na mabishano kati ya maafisa mbali mbali wa usalama wakati marais Idriss Deby wa Chad, Alassane Outara na waziri mkuu wazamani wa Ethopia Hailemariam Desalegn walipokuwa wanaingia. Haijafahamika kile kilichosababisha mabishano hayo

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG