Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Agosti 03, 2021 Local time: 15:48

WHO : Katazo la wasafiri kutoka China kuepusha maambukizo linaweza kufeli


Waislam India wavaa vitambaa kufunika pua na midomo wakati wa sala ya Ijumaa kujilinda na kirusi corona msikitini huko Ahmadabad, India, Jan. 31, 2020.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kuwa katazo la kusafiri kudhibiti kuenea kwa kirusi korona ambacho ni kipya kilichoibuka China linaweza kufeli na kupelekea hali ya kuenea kwa janga hilo kuwa mbaya zaidi duniani.

Ripoti za hivi karibuni zinaonyesha idadi iliyothibitishwa ya wagonjwa wenye kirusi hicho kukaribia 12,000, ikiwemo vifo 259, na wagonjwa wengi kati ya hao na vifo vyote vimetokea China.

Kamati ya masuala ya dharura ya WHO imetangaza kuwa kirusi corona ni tishio la afya ya umma ulimwenguni Alhamisi, na kuibua mapendekezo kadhaa yanayo kusudia kupunguza kasi ya kuenea kwa ugonjwa huo.

WHO haipendekezi kuweka zuio lolote la kusafiri na biashara pamoja na kuwepo ongezeka la kasi la ugonjwa huo nchini China na haupungui, lakini unaendelea kuenea ulimwenguni. Zaidi ya watu 100 wameripotiwa kuwa na ugonjwa huo katika nchi nyingine 22.

Ili kukabiliana na hali hiyo, baadhi ya mashirika ya ndege yamesitisha safari zake kwenda China bara. Marekani, ambayo imetangaza maambukizo ya kirusi corona kuwa ni dharura ya umma, inasema itazuia wageni kuingia nchini humo ambao hivi karibuni walikuwa wametembelea China. Australia inasema itachukuwa hatua kama za Marekani.

Msemaji wa WHO Christian Lindmeier, anasema kufunga mipaka hakuwezi kuzuia kirusi hicho kuingia katika nchi nyingine

“Kama sote tunavyojua katika matukio mengine ya maambukizi, iwe Ebola au magonjwa mengine, pale watu wanapotaka kusafiri, watafanya hivyo. Na iwapo njia rasmi za kupita zikiwa zitafungwa, watapita katika njia za panya,” amesema Lindmeier.

“Lakini njia pekee ya kudhibiti maambukizo, kupima iwapo mtu ana homa, kwa mfano, kutambua historia ya safari yake, kujaribu kufuatilia nani anapita katika mpaka wako na kuona iwapo wana dalili zozote za maambukizo ni kupitia mipaka rasmi.

Lindmeier anasema nchi zinahaki ya kiutawala kuchukua hatua zozote wanazoamini ni bora katika kuwalinda raia wao wasipate maambukizo.

“Hata hivyo mapendekezo yatafuatwa. Na, iwapo katazo la kusafiri litatolewa, tunatarajia kuwa litakuwa la muda mfupi iwezekanavyo ili watu waweze kuendelea na maisha yao vyema kwa kadiri itakavyowezekana,” amesema Lindmeier.

“Lakini bila shaka, tuongeze uangalizi na ufuatiliaji ili kuepuka kuenea kwa ugonjwa huo.”

China inachukuwa hatua kali kuzuia kuenea kwa kirusi corona. Mji wa Wuhan, ambapo ni chimbuko la ugonjwa huo na miji mingine 15 imewekewa karantini, na watu takriban milioni 50 wamekatazwa kutoka nje.

Pamoja na juhudi hizo, kirusi hicho bado kinaendelea kuenea kwa kasi.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG