Lavrov alitua mjini Cairo Jumamosi alasiri, kituo cha kwanza cha safari yake ya bara la Afrika ambayo itampeleka Ethiopia, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kulingana na shirika la serikali la RT la Russia.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri ilisema Waziri wa anayeongopza wizara hiyo, Sameh Shukry, alifanya mazungumzo na Lavrov Jumapili asubuhi.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Russia alipangiwa kukutana baadaye Jumapili na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Ahmed Aboul Gheit. Pia atahutubia wawakilishi wa kudumu wa shirika la pan-Arab, kwa mujibu wa shirika hilo la habari.
Vita vya Russia nchini Ukraine vimekuwa na athari mbaya kwa uchumi wa dunia, na kusababisha bei ya mafuta na gesi kupanda kwa viwango ambavyo havikuwa vimeshuhudia awali.
Ukraine ni miongoni mwa nchi zinazosafirisha ngano, mahindi na mafuta ya alizeti duniani, lakini uvamizi wa Russia dhidi ya nchi hiyo na kufungwa kwa bandari zake kumeathiri mchakato wa usafirishaji wa bidhaa.