Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Novemba 15, 2024 Local time: 05:58

Israel yaitaka Russia kuomba radhi baada ya waziri wake wa mambo ya nje kudai Hitler alikuwa na asili ya Kiyahudi


Waziri wa mambo ya nje wa Russia Sergei Lavrov akihudhuria mkutano wa waandishi wa habari baada ya kufanya mazungumzo na wawakilishi wa mataifa ya Kiarabu mjini Moscow, April 4, 2022. Picha ya Reuters
Waziri wa mambo ya nje wa Russia Sergei Lavrov akihudhuria mkutano wa waandishi wa habari baada ya kufanya mazungumzo na wawakilishi wa mataifa ya Kiarabu mjini Moscow, April 4, 2022. Picha ya Reuters

Israel Jumatatu imemkosoa vikali waziri wa mambo ya nje wa Russia Sergei Lavrov baada yake kudai kwamba Adolf Hitler alikuwa na asili ya Kiyahudi, ikisema huo ni “uongo” usiosameheka ambao umepuuza maovu yaliyotendwa na Wanazi dhidi ya Wayahudi.

Viongozi wa mataifa kadhaa ya magharibi wamelaani matamshi ya waziri wa mambo ya nje wa Russia, huku Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy akiishtumu Russia kwa kusahau mafunzo ya vita vya pili vya dunia.

Katika ishara ya kuzorota kwa uhusiano kati ya Israel na Moscow, wizara ya mambo ya nje ya Israel imemuita balozi wa Russia nchini humo na imeitaka Russia kuomba radhi.

“Uongo huo unalenga kuwashtumu Wayahudi wenyewe kwa uhalifu wa kutisha katika historia waliotendewa,” waziri mkuu wa Israel Naftali Bennet amesema katika taarifa.

Lavrov alitoa madai hayo Jumapili kwenye televisheni ya Italy alipoulizwa kwa nini Russia ilisema inataka kuondoa hisia za Kinazi nchini Ukraine, wakati Rais wa Ukraine mwenyewe, Volodymyr Zelenskiy ni Myahudi.

“Wanaposema ni hisia gani hizo za Kinazi wakati sisi wenyewe ni Wayahudi, nadhani kwamba Hitler pia alikuwa na asili ya Kiyahudi, kwa hivyo haimaanishi chochote,” Lavrov alikiambia kituo cha televisheni Rete channel 4, akizungumza kupitia mkalimani raia wa Italy.

Zelenskiy, katika ujumbe wake wa kila usiku kwa njia ya video amesema kuwa Moscow imekaa kimya tangu Lavrov alipotoa matamshi hayo.

“Hii ina maana kwamba uongozi wa Russia umesahau mafunzo yote ya vita vya pili vya dunia,” amesema, akiongeza “au pengine hawajawahi kupata mafunzo hayo.”

XS
SM
MD
LG