Kwa mjibu wa asasi za kiraia, mapigano hayo kati ya makabila ya Wanyamulenge, Wafulero, Wabembe na Banyindu yalipamba moto mwishoni mwa juma, baada ya kundi la wanamgambo wa Nyamulenge kumshambulia na kumua mkuu moja wa kijiji kutoka kabila la Wafulero.
Mkuu wa Wilaya ya Fizi, Aime Mutipula Kawaya amethibitisha habari hiyo, na kusema kwamba maelfu ya wakazi kutoka makabila hayo walikimbilia msituni ambapo hawana huduma yoyote kwa hivi sasa.
Kiongozi moja wa shirika la kiraia katika kijiji cha Minembwe, Rugira Nyagatetera ameiambia Sauti ya Amerika kwamba Jumatatu, kuna vijiji kadhaa vilivyochomwa moto na watu wasiojulikana, na kwamba hadi sasa kuna watu wasiojulikana idadi yao ambao wameuawa katika ghasia hizo.
Wawakilishi wa makabila hayo hasimu walikutana mjini Bukavu mwishoni mwa Juma kwa lengo la kutafuta suluhisho la mgogoro huo. Walitoa wito kwa serikali kuu kuingilia kati mgogoro huo ili kurejesha amani na usalama katika wilaya ya Fizi.
Mkuu wa wilaya huyo ameiambia Sauti ya Amerika kwamba Jumanne hii atakutana mjini Uvira na viongozi wa kijeshi na Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa mataifa, MONUSCO, ili kutafuta mbinu za kukomesha ghasia hizo za kikabila katika wilaya ya Fizi.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Patrick Nduwimana, Washington, DC.
Facebook Forum