Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Novemba 28, 2022 Local time: 21:11

DRC: Mji wa Kisangani wakabiliwa na mgao wa umeme


Kisangani, DRC

Sehemu kubwa ya mji wa Kisangani mji wa tatu kwa ukubwa DRC, haina umeme tangu Alhamisi iliopita.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mamlaka ya huduma za umeme DRC, SNEL, ukosehu huo wa umeme umesababishwa na kuharibika kwa injini mbili zinazosaidia bwawa la maji la Kisangani linalozalisha umeme.

Taarifa hizo zinasema, hivi sasa injini moja pekee ndiyo inafanya kazi. Kufuatia hali hiyo, kiwango cha nguvu za umeme kimeshuka kutoka kwenye megawati 10 hadi megawati 3 na hivyo kuilazimu mamlaka ya umeme kuanzisha mgao katika kutoa huduma hiyo.

Wakazi wa mji wa Kisangani wanalalamika wakisema uhaba wa umeme umezorotesha shuguli nyingi kwenye viwanda, hospitali na zahanati, na imeleta hofu kubwa kwa wakazi wa Kisangani wanaotumia chakula kinachohifadhiwa kwenye jokovu.

Makolo Kotambula, mkazi wa mji wa Kisangani ameiambia Sauti ya Amerika kwamba, moja ya athari kubwa ya mgao huo ni kuwa vyumba vya kuhifadhi maiti kwenye baadhi ya hospitali havifanyi kazi.

Mamlaka ya umeme SNEL imesema katika taarifa yake kwamba, wakati shughuli za ukarabati wa injini zilizoharibika zikiendelea, kiwango kidogo cha umeme kinachopatikana kitapelekwa kwenye vituo muhimu, hususani hospitali na zahanati.

Mamlaka hiyo imeahidi kuwa katika kipindi cha wiki moja, umeme utakuwa umerudi katika mji wa Kisangani.

Wakazi wa Kisangani wanaiomba serikali kuu kununua injini mpya na kukarabati bwawa la mji wa Kisangani.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Patrick Nduwimana, Washington, DC.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG