Shambulizi hilo limesababisha khofu kubwa kwa watu wengi ikiwemo waumini katika makanisa na viongozi wao.
Picha za shambulizi hilo zilizobandikwa katika mitandao ya kijamii zinaonyesha miili iliyokuwa na damu ikiwa imelala kwenye kanisa hilo.
Wengi wa waliojeruhiwa wanatibiwa katika hospitali. Washambuliaji walilenga Kanisa Katoliki la St. Fransis katika jimbo la Ondo wakati waumini walipokuwa wamekusanyika Jumapili wakiadhimisha siku ya Pentekoste, amesema mbunge Ogunmolasuyi Oluwole.
Miongoni mwa waliokufa ni pamoja na watoto. Bado haijafahamika haraka nani aliyehusika na shambulizi hilo katika kanisa. Wakati Nigeria ikiwa inataabika na maswala ya kiusalama, Ondo ni jimbo linalojulikana kuwa ni eneo lenye amani nchini humo.
Jude Arogundale askofu katika Kanisa Katoliki Dayosisi ya Ondo anaeleza “Si jambo la kuamini kwamba mtu anaweza kuja na nia ya makusudi ya kuuwa watu wote ndani ya kanisa. Na wale waliokuwa wanakimbia walipigwa risasi nje, waliokuwa ndani walipigwa risasi wakiwa ndani. Walirusha kilipuzi kwa ajili ya kubomoa madhabahu . tukio kama hili baya linaweza kufanywa na muovu.”
Nigeria inakabiliwa na ghasia mbaya za makundi yenye silaha. Kote nchini watu wana wasiwasi kuhusu uwezo wa serikali kukabiliana na kiwango cha hali ya kutokuwa na usalama