Jeshi la Mali lilisema wanajeshi wanane waliuawa wakati wa shambulio katika eneo la magharibi mwa taifa hilo la Sahel ambako wanajihadi wanaendesha operesheni zao, na hivvo kuongeza mara mbili idadi ya waliouawa hapo awali.
Katika taarifa yake mpya Alhamisi jioni, jeshi la Mali lilisema wanajeshi saba walijeruhiwa pia katika shambulio la Jumanne, magari mawili ya kijeshi yaliharibiwa, na kuongeza kuwa washambuliaji 31 waliuawa, bila ya kulitaja kundi la washambuliaji.
Likiripoti kwa mara ya kwanza kuhusu shambulio hilo siku ya Jumatano, jeshi lilisema wanajeshi wanne walifariki na darzeni ya wengine kujeruhiwa wakati kikosi katika eneo la NARA kililengwa katika shambulio kali sana lililojumuisha vilipuzi vilivyotengenezwa kienyeji na silaha nzito.
Katika taarifa yake ya Alhamisi, jeshi lilisema miili 31 ya washambuliaji iligunduliwa Alhamisi asubuhi, pamoja na silaha na zana nyingine. Lakini jeshi halikusema ni kundi gani lilifanya shambulizi.
Mali ni kitovu cha uasi wa wanajihadi ambao ulianzia kaskazini mwa nchi hiyo mwaka 2012 na kuenea hadi nchi jirani za Niger na Burkina Faso.