Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Juni 13, 2024 Local time: 14:01

Wabunge wa upinzani wanadhulumiwa sana - Ripoti


Utafiti wa wabunge 300 kutoka nchi 19 umegundua kwamba vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu, mkiwemo mateso ya kimwili, ubakaji, mateso na ukamataji kiholela wa wabunge wa upinzani vimeongezeka maradufu.

Shirikisho la mabunge limeelezea mjini Geneva katika ripoti mpya hoja yake kuhusu madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya wabunge wa upinzani katika nchi zilizoanda uchaguzi hivi karibuni au ambazo zinajianda kufanya uchaguzi.

Shirikisho hilo linasema darzeni ya wabunge wa upinzani walikandamizwa kwa kunyimwa uhuru wa kujieleza na kufanya mikutano.

Ripoti hiyo inasema ukamataji kiholela, kuachiwa huru na kukamatwa tena kwa wapinzani imekua mbinu ya vitisho inayotumiwa na vyombo vya dola.

Mfano, polisi ya Uganda ilimkamata na kumuachia mara kadha mbunge wa upinzani maarufu Bobi Wine, tukio la karibuni ni jumanne wiki hii, ambapo inadaiwa kuwa polisi walimpulizia gesi ya kutoa machozi akiwa ndani ya gari lake. Bobi Wine alikataliwa kuanda mikutano kwa madai kwamba atavuruga usalama wa umma.

Shirikisho la mabunge lilifwatilia kesi za wabunge 9 wa upinzani nchini Ivory Coast ambao walikamatwa na kuzuiliwa kinyume cha sheria kwa mashtaka ya kusababisha vurugu na kusambaza habari za uongo.

Shirikisho hilo linasema hakuna Ushahidi unaonyesha kuwa wana hatia, na mashtaka dhidi yao yaonekena kuchochewa na sababu za kisiasa, kutokana na uchaguzi uliofanyika nchini Ivory Coast hapo tarehe 31 Oktoba.

Shirikisho hilo (IPU) limekua likifwatilia kwa karibu hali inayojiri Venezuela kwa miaka mingi. Msemaji wa IPU Thomas Fitzsimons ameiambia Sauti ya Amerika kwamba, kiwango cha vitisho wanavyopitia wapinzani nchini Venezuela, kitafanya uchaguzi wa wabunge wa tarehe 6 Disemba usiwe huru na wa haki.

“Wengi miongoni mwa wabunge wa upinzani 134 walioshambuliwa, kunyanyaswa au kufanyiwa vitisho. Kama nilivyosema, wanaweza kunyanyaswa kwenye mitandao ya kijamii au kutendewa mateso ya kimwili.

Kwa hiyo, kuna vigezo tofauti vya vitisho. Naweza kusema kwamba wanafanyiwa vitisho kwa njia mmoja ama nyingine.” Amesema Thomas Fitzsimons

Fitzsimons anasema kesi mpya ya kutisha inamuhusu mbunge wa upinzani nchini Zimbabwe Joana Mamombe. Anasema mbunge huyo alizuiliwa mwezi Mei baada ya kushiriki maandamano ya kuomba ulinzi zaidi kwa watu maskini wakati wa janga la corona.

“nchi ilikua chini ya masharti ya kufunga shughuli zote, kwa hiyo alikamatwa kwa madai hayo. Akiwa gerezani, ripoti tulizosikia ni kwamba aliteswa, na kufanyiwa ukatili wa dhulma ya kingono.

Kwa hiyo, tuna wasiwasi mkubwa kutokana na taarifa hiyo.”

Fitzsimons anasema Mamombe aliachiliwa kwa dhamana na baadae akakamatwa tena. Anasema vitisho vya mara kwa mara kuwazuia, kuwaacia huru na kuwakamata tena wapinzani, ni mbinu inayotumiwa na viongozi walioko madarakani kudhoofisha upinzani ili kusalia madarakani. Hakuna maelezo yaliotolewa na nchi zilizotajwa katika ripoti ya IPU.

Imetayarishwa na Patrick Nduwimana, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG