Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Septemba 15, 2024 Local time: 12:55

Upinzani wapania kupambana na “udikteta” Tanzania


Viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani na wadau wengine walipokutana Zanzibar, Jumanne, Disemba 18, 2018.
Viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani na wadau wengine walipokutana Zanzibar, Jumanne, Disemba 18, 2018.

Vyama vya siasa vya upinzani nchini Tanzania vimetangaza kuwa mwaka 2019 utakuwa ni mwaka wa kudai demokrasia nchini humo na kupigania uchumi ulioanguka.

Viongozi wa upinzani waliokutana Zanzibar Jumanne wamesema katika tamko lao kuwa Tanzania hivi sasa ina mmomonyoko wa demokrasia na kuna ishara zote za utawala wa udikteta, usiojali haki za kisiasa, kijamii pamoja na za kiuchumi kwa wananchi.

Viongozi wa vyama sita

Tamko hilo lililotiwa saini na viongozi wa vyama sita vya upinzani limeahidi na kuwataka wananchi wa Tanzania kujitolea katika jitihada za kupambana kudai haki.

“Tutaendelea kudai haki zetu zote tunazonyimwa kinyume na sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Uchumi kuanguka

Viongozi hao wamedai bila kutoka takwimu kwamba uchumi wa Tanzania umeanguka kwa kiasi kikubwa chini ya utawala wa rais John Magufuli na kwamba hali hiyo inaumiza zaidi wananchi masikini.

“Pamoja na juhudi za propaganda za serikali kuonyesha kuwa hali ya uchumi ni nzuri kinyume na hali mbaya iliyoko, tunaona ni muhimu kueleza kwa uwazi kuwa baada mwelekeo mzuri kiasi wa hali ya uchumi wa nchi yetu kwa miaka kumi, hali ya uchumi wetu imeharibika katika kipindi cha miaka hii mitatu tu ya awamu ya tano.”

Uratibu wa mikutano ya hadhara

Tamko hilo limeendelea kusema “Kama vyama vya siasa vyenye uhalali na vyenye utaratibu uliowekwa rasmi kisheria na kikatiba, tutatangaza rasmi namna na utaratibu wa kufanya mikutano yetu ya hadhara katika kila kona ya nchi yetu, hatutaruhusu katazo haramu na lisilo na mashiko ya kisheria litumike kutuzuia kutekeleza wajibu wetu.”

Wapinzani hao wamesema serikali ya Rais Magufuli imekuwa ikiendeleza vita dhidi ya vyama vya upinzani pamoja na wote wanaonekana wana mawazo mbadala juu ya namna nchi yetu inavyoendeshwa, ingawa katiba ya nchi inalinda mfumo wa vyama vingi.

Rais Magufuli

Mara tu baada ya kuingia madarakani mwaka 2015 serikali ya Rais Magufuli ilipiga marufuku mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ikisema kwamba muda wa kampeni umekwisha

“Imekuwa ni kawaida sasa kwa Mkuu wa Nchi yetu, pamoja na wafuasi wake, kuwaita viongozi na wanasiasa wa vyama vya upinzani, pamoja na wakosoaji wa serikali kuwa ni ‘Mawakala wa Nchi za Nje’ na si Wazalendo,” tamko la vyama hivyo sita vilivyosaini tamko hilo.

Kutekwa na kukamatwa wanasiasa

Mambo mengine yaliyozungumziwa katika mkutano huo ni pamoja na madai ya kutekwa na kukamatwa kwa wananchi, wakiwemo viongozi wa kisiasa, waandishi wa habari na wafanyabiashara, kuokotwa kwa miili ya watu kwenye fukwe mbalimbali nchini; jaribio la kuuawa kwa Mbunge Tundu Lissu na hatua ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama kukataa kufanya uchunguzi wowote wa maana juu ya tukio hilo; uwepo wa sheria mbaya za Habari na Takwimu, pamoja na uletwaji wa kanuni za uendeshwaji wa Asasi za Kiraia (AZAKI), Kanuni za Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Mswada wa mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa ambao umewasilishwa bungeni hivi karibuni.

Freeman Mbowe

Mkutano ulitaja pia kukosekana katika mkusanyiko huo kiongozi wa kambi upinzani bungeni, Freeman Mbowe ambaye anashikiliwa gerezani baada ya kukosa dhamana katika kesi ya uchochezi wa kisiasa inayomkabili.

Tundu Lissu

Mbunge Tundu Lissu ambaye alikuwa msemaji mkuu wa upinzani nje na ndani ya bunge la Tanzania angali nchini Ubelgiji ambako anapata matibabu tangu kushambuliwa kwa risasi mwaka mmoja uliopita mjini Dodoma.

Tamko lasainiwa

Viongozi wa upinzania waliohudhuria mkutano wa Zanzibar na kutia saini tamko la mkutano huo ni Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu, CUF, James Francis Mbatia, Mwenyekiti Taifa, NCCR Mageuzi, Oscar Emanuel Makaidi, Mwenyekiti Taifa, NLD, Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar, CHADEMA, Hashim Rungwe Spunda, Mwenyekiti Taifa, CHAUMMA na Kabwe Zitto, Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo

XS
SM
MD
LG