Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 26, 2024 Local time: 03:51

CPJ yataka Tanzania ichunguze kupotea kwa Azory Gwanda


Picha ya Azory Gwanda katika magazeti baada ya kupotea kwake November 2017
Picha ya Azory Gwanda katika magazeti baada ya kupotea kwake November 2017

Mwaka mmoja baada ya kupotea kwa mwandishi wa habari wa kujitegemea Azory Gwanda nchini Tanzania, kamati inayotetea waandishi wa habari, CPJ, imerudia wito wake kwa serikali ya Tanzania kufanya uchunguzi wa kuaminika ifahamike kilichomtokea.

Katika taarifa iliyotolewa na makao makuu ya CPJ mjini New York Jumatano kamati hiyo ya kimataifa imesema serikali ya Tanzania haina budi kutekeleza ahadi yake ya kufanyia uchunguzi kamilifu wa kupotea kwa mwandishi huyo.

Gwanda, ambaye alikuwa akiandikia magazeti binafsi ya Mwananchi na The Citizen alipotea Novemba 21, 2017. Mke wake, Anna Pinoni, aliripoti kumwona Gwanda akiondoka katika shamba lao katika mkoa wa Pwani na watu ambao hawakutambulika katika gari jeupe aina ya Land Cruiser. Gwanda alimwambia mke wake kwamba anakwenda katika safari ya dharura na atarejea siku iliyofuata. Hajaonekana tena tangu wakati huo.

Kulingana na gazeti la The Citizen Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania Kangi Lugola alipuuzia kupotea kwa Gwanda alipoulizwa Julai mwaka huu, na siku chache baadaye aligusia huenda aliondoka nyumbani kwa sababu ya matatizo ya kifamilia.

"Ukosefu wa uchunguzi wa kuaminika kuhusiana na kupotea kwa mwandishi wa habari Azory Gwanda ni jambo la kusikitisha sana, na linaashiria sababu ya wasiwasi wetu kuhusu uhuru wa vyombo vya habari Tanzania,” alisema Angela Quintal, Mratibu wa CPJ wa Afrika.

Quintal na mwakilishi wa CPJ katika nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara, Muthoki Mumo, walitembelea Tanzania mapema Novemba 2018 kukutana na waandishi wa habari na kupata maelezo zaidi ya changamoto wanazokabiliana nazo. Jioni ya Novemba 7 maafisa wa serikali walifika katika hoteli yao na kuwachukua, kuwahoji kwa saa kadha kuhusu utafiti wao na kudai kuwa walikuwa wamekiuka masharti ya viza zao.

Waliondoka nchini humo siku moja baadaye.

XS
SM
MD
LG