Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 20, 2024 Local time: 04:27

Trump akanusha tuhuma mpya kuwa Putin anamdhibiti


Rais Donald Trump (kushoto) na Rais Vladimir Putin (kulia)
Rais Donald Trump (kushoto) na Rais Vladimir Putin (kulia)

Rais Donald Trump amekanusha ripoti za vyombo vya habari zinazo eleza amedhibitiwa na Russia, pia na Rais Vladimir Putin au anaficha masuala yanayohusu maongezi yake ya siri na kiongozi wa Russia walipo kutana mara tano, ikiwemo mkutano wao wa Julai huko Helsinki.

Alipoulizwa moja kwa moja Jumamosi jioni na kituo cha habari cha Fox News katika kipindi kinacho endeshwa na Jeanine Pirro iwapo hivi sasa au wakati wowote amewahi kushirikiana na Russia, Trump amesema, “ Nafikiri hili jambo linaniumiza zaidi kuliko yote, jambo ambalo sijawahi kuulizwa.”

Kiongozi huyo wa Marekani amesema, “Iwapo utawauliza wananchi wa Russia, Mimi nimekuwa mwenye msimamo mkali zaidi kuliko mtu yeyote, yeyote yule – pengine kuliko kipindi cha rais yoyote mwengine, lakini bila shaka marais watatu au wanne wa mwisho, marais wa zama hizi. Hakuna kati yao aliyekuwa na msimamo mkali kama nilivyo mimi katika masuala yeyote yale.

Trump alikuwa anajibu ripoti ya gazeti la The New York Times. Ripoti hiyo inaeleza kuwa maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (FBI) walianza kuchunguza iwapo Trump “ alikuwa anafahamu anashirikiana na Russia au bila ya kujua aliangukia katika ushawishi wa Moscow” kwa sababu walikuwa wameshtushwa sana na tabia ya Trump baada ya kumfukuza kazi mkuu wa FBI wa zamani James Comey Mei 2017, wakati alipokuwa akiongoza uchunguzi juu ya Russia kuingilia kati uchaguzi wa rais wa Marekani 2016.

“Ni jambo ovu kabisa walilosema…,” Trump amesema. “Wao kwa kweli ni gazeti linalo leta maafa mkubwa.”

Wakati huohuo Kamati ya Baraza la Bunge la Marekani -Congress litafanya tathmini ya ripoti ya gazeti moja ilioandika kuwa Shirika la Upelelezi wa Makosa ya Jinai, FBI, lilichunguza iwapo Rais Donald Trump amekuwa akiwatumikia Russia katika wadhifa wake wa urais, dhidi ya maslahi ya Marekani, mwenyekiti wa jopo hilo Mdemokrat amesema Jumamosi.

Gazeti la New York Times limeripoti kuwa uchunguzi huo ulianza kufanywa mara baada ya Trump kumfukuza kazi James Comey wakati akiwa mkurugenzi wa FBI, mwezi Mei, 2007, na kusema kuwa wachunguzi hao walioteuliwa kutoka idara hiyo ilibidi watafakari iwapo vitendo vya Trump vilikuwa vinatishia usalama wa taifa.

White House Ijumaa jioni ilikanusha habari zilizo andikwa katika gazeti la Times kwa kuziita ni “upuuzi,” wakati Trump siku ya Jumamosi aliwashambulia Comey na FBI kwa dazeni ya lawama kupitia ujumbe wa tweet.

Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria ya Bunge Jerrold Nadler amesema jopo lake “litachukuwa hatua ili kufahamu zaidi mambo yote mawili; vitendo vya rais na hatua walizo chukuwa FBI kukabiliana na vitendo hivyo” katika wiki zijazo.

Amesema pia wawakilishi watatafuta njia ya kuwalinda wachunguzi kutokana na “kuendelea kwa lawama za kiholela” anazotoa rais.

“Hakuna sababu ya kutilia mashaka weledi na usimamizi thabiti wa wafanyakazi wa FBI, mashaka ambayo rais ameyaonyesha kutokana na kukerwa kwake na habari hii iliyo chapishwa katika gazeti,” Nadler, Mdemokrat wa New York, amesema katika tamko lake.

“Tumekuja kufahamu kutokana na ripoti hii kuwa hata hapo siku za awali za uongozi wa Trump, mwenendo wa rais ulikuwa hauaminiki na unatia wasiwasi mkubwa na hivyo FBI ikalazimika kuchukua hatua ya kipekee – kwa kuanzisha uchunguzi dhidi ya rais aliyekuwa madarakani,” Nadler amesema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Congress Adam Schiff amesema hawezi kutoa maoni yake juu ya maudhui ya ripoti hii, lakini amesema kamati yake itaweka shinikizo kuanzia sasa kwa kufanya uchunguzi juu ya mahusiano ya Trump na Russia.

Mchunguzi Maalum wa Marekani Robert Mueller alianza kufuatilia uchunguzi uliokuwa umeanzishwa dhidi ya Trump masiku kadhaa baada ya FBI kufungua uchunguzi huo, akiwa na tathmini madai ya kuwa Russia iliingilia kati uchaguzi, gazeti la Times liliripoti. Russia imekanusha ilijaribu kuingilia uchaguzi huo.

Trump amejibu siku ya Jumamosi kwa kushambulia gazeti la Times na viongozi wa zamani wa FBI na kukosoa uchunguzi wa awali uliofanywa na idara hiyo juu ya Mdemokrat Hillary Clinton, hasimu wake wa kisiasa katika uchaguzi wa 2016.

“Ushindi, nimejua hivi punde kupitia gazeti linalo feli la New York Times kwamba viongozi wa zamani mafisadi wa FBI, ambao takriban wote walifukuzwa kazi au kulazimishwa kujiuzulu kutoka katika idara hiyo kwa sababu mbalimbali mbaya, walianzisha uchunguzi dhidi yangu, bila sababu yeyote na bila ya ushahidi wowote, baada ya kumfukuza kazi mwongo James Comey, fisadi mkubwa!” Trump alituma ujumbe huu wa tweet.

XS
SM
MD
LG